*********************
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeteketeza bidhaa za aina mbalimbali zenye viambato sumu ambazo hazikidhi matakwa ya viwango za uzito wa tani tisa zenye thamani ya shilingi milioni 400.
Akizungumza Mkuranga mkoani Pwani Kaimu Mkurugenzi wa Usimamizi na Utekelezaji wa Sheria TBS, Dkt, Candida Shirima, amesema kuwa shehena ya bidhaa zilizoteketezwa zina uzito wa tani 9 na nyingi ni vipodozi vyenye viambata sumu ambayo vimeshapingwa marufuku kwa mujibu wa sheria ya viwango sura 130.
Dkt Shirima amesema kuwa viambata sumu hivyo ni aina ya Zebaki,hydroquinone na steroids ambayo ni hatari kwa afya ya watumiaji wa vipodozi kwani husababisha madhara mbalimbali kama vile ya ngozi muwasho, ngozi kuwa nyekundu, laini,saratani madhara ya figo na uzazi.
Aidha ameitaka jamii kuepuka kutumia vipodozi vyenye viambata sumu na vilivyopigwa marufuku kama ambavyo imekuwa ikishauriwa na kusisitizwa na mamlaka hiyo pamoja na wataalamu wa afya ili kulinda afya.
Pia amewataka wananchi kuangalia muda wa matumizi kwenye bidhaa hususani vyakula kabla ya kununua au kuzitumia huku wafanyabishara kuhakikisha kuwa wanazingatia sheria na kanuni na viwango ili kutoingiza nchini,kuzalisha,kuuza au kusambaza bidhaa zisizokidhi vigezo vya ubora na usalama ili kuwalinda watumiaji na kukuza uchumi wa nchi.
Kwa upande wake Kaimu Meneja Kanda ya Mashariki wa TBS, Fransis Mapunda amesema kuwa bidhaa hizo zilizotekezwa wamezikamata katika maeneo mbalimbali ikiwemo mkoani Morogoro, Dar es Salaam na Pwani huku akiwataka wafanyabishara kutokujihusisha na bidhaa zisizokidhi vigezo.
“Zoezi la ukaguzi ni endelevu katika maeneo yote hivyo sehemu yoyote mtu atakayejihusisha na biashara ambazo hazikidhi matakwa ya sheria atakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria kwa mujibu wa sheria zilizowekwa kwa masilahi mapana ya taifa kwa ujumla”amesema Mapunda