***********************
Na Lucas Raphael Tabora
Shahidi wa kwanza katika shauri la Madai linalomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Tabora Kitwala Komanya ameiambia Mahakama kuwa anadai alipwe fidia ya shilingi milioni 140 kutokana na vitendo vya udhalilishaji alivyofanyiwa na Januari 05/2021.
Akitoa ushahidi wake mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Tabora Demetrio Nyakunga huku akiongozwa na wakili wake Kelvin Kayaga alisema kuwa siku hiyo mdaiwa alimfanyia vitendo vinavyodhalilisha utu wake mbele ya familia yake na majirani zake.
Shahidi huyo Alex Ntonge ambaye ndiye mdai wa kesi namba 04/2021 ameiambia Mahakama kuwa mdaiwa alifika nyumbani kwake akiwa askali polisi wanne wawili wakiwa na bunduki alimwamuru apige magoti kwa takribani dakika 45 nje mbele ya nyumba yake.
Ntonge aliongeza kuwa pia mdaiwa alimwamuru alale kifudifudi ndani ya gari la Polisi huku akiwa ameelekezewa mitutu ya bunduki huku akimtolea maneno ya kashfa yasiyo na staha mbele ya jamii.
“ Nilitii maagizo ya kupiga magoti chini, kulala kifudifudi ndani ya gari la polisi na kupelekwa mahabusu bila kosa kutokana na kuhofia uhai wangu’’ alisema Shahidi huyo.
Katika dai lake la pili la kushitakiwa kwa nia hovu shahidi huyo alisema kuwa januari 06/2021 alifikishwa mbele ye hakimu Mfawidhi wa mahakama ya Mwanzo ya mjini Tabora kwa tuhuma za kumtukana mkuu huyo wa wilaya wa zamani kwa njia ya Mtandao.
Ntonge ameiambia mahakama hiyo kuwa katika kesi hiyo ya jinai namba 07/2021 mdaiwa Kitwala komanya alitakiwa kuleta ushahidi lakini hakutekeleza matakwa ya mahakama ikabidi shauri hilo liondolewe na yeye kuachiliwa huru.
Akijibu hajo za wakili Issa Rajab Mavula ambaye anamwakilisha mdaiwa shahidi huyo alisema akuweza kuwashitaki polisi waliohusika kumkamata kwa vile wao walipokea maelekezo ya Mkuu wa Wilaya.
Ntonge anadai alipwe nafuu ya shilingi milioni 80 kutokana na kuzuia uhuru wake, shilingi milioni 30 kwa kumshitaki kwa nia hovu pamoja na tshs milioni 30 kwa kumdhalilisha utu wake.
Kesi hiyo imehairishwa hadi oktoba 03/2022 ambapo itaendelea kusikilizwa kwa upande wa mdai kuleta mashaidi wengine.