Ujumbe wa Serikali ya Tanzania ukiongozwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Prof. Jamal Katundu kwa kushirikiana na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab ukiwa katika mazungumzo na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kazi Qatar, Mhe. Mohammed Hassan Al-Obaidly Jijini Doha Tarehe 29 Agosti,2022
Kikao baina ya ujumbe wa Serikali ya Tanzania na ujumbe kutoka Wizara ya Kazi nchini Qatar kikiendelea Jijini Doha
Ujumbe wa Serikali ya Tanzania na ujumbe kutoka Wizara ya Kazi nchini Qatar ukiwa katika picha ya pamoja baada ya kumaliza kikao chao Jijini Doha
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Prof. Jamal Katundu akimueleza jambo Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Elimu ya Juu Qatar Mhe. Ibrahim bin Saleh Al Nuaimi wakati ujumbe wa Serikali ya Tanzania ulipofanya ziara katika Ofisi za Wizara hiyo Jijini Doha. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab akimkabidhi zawadi Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Usafirishaji ya MOWASALAT ya Qatar wakati ujumbe wa Tanzania ulipofanya ziara katika Ofisi hizo Jijini Doha
***********************
Ujumbe wa Serikali ya Tanzania unaoongozwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Prof. Jamal Katundu kwa kushirikiana na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab umeendelea na ziara nchini Qatar ambapo umekutana na kuzungumza na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kazi Qatar, Mhe. Mohammed Hassan Al-Obaidly jijini Doha tarehe 29 Agosti,2022.
Viongozi hao wamejadiliana namna bora ya kuendelea kutekeleza Mkataba wa Ajira uliosainiwa kati ya Tanzania na Qatar mwaka 2014. Tanzania inaangalia namna ya kupata nafasi za ajira kwa Watanzania ili waende kufanya kazi nchini humo.
Mhe. Al-Obaidly amesema Serikali ya Qatar imeanza mchakato wa kuanzisha Kituo Maalum cha Visa (Visa Center) nchini Tanzania ili kurahisisha namna ya kupata Watanzania watakaokwenda kufanya kazi nchini Qatar.
Ikiwa Kituo hicho kitaanzishwa nchini Tanzania kitakuwa cha kwanza kujengwa barani Afrika ambapo vituo kama hivyo vipo katika nchi za India na Ufilipino nchi ambazo zinatoa idadi kubwa ya wafanyakazi kwenda kufanya kazi nchini Qatar.
Kuanzishwa kwa kituo hicho kitafungua fursa nyingi za ajira na kurahisisha upatikanaji wa nafasi za ajira kwa Watanzania. Mhe. Al-Obaidly ameahidi kuwa serikali ya Qatar itaendelea kushirikiana na Tanzania ili kupata Watanzania wenye sifa za kuajiriwa nchini humo kwa kutumia mifumo ya ajira ya nchi hiyo.
“Tutashirikiana na Tanzania kupata wafanyakazi wenye ujuzi wa fani mbalimbali ambao wana uzoefu na nidhamu ili waweze kupata nafasi za ajira nchini humu”, alisema Mhe. Al-Obaidly
Kwa upande wake, Balozi Fatma Rajab aliihakikishia Serikali ya Qatar kuwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki itaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha ili kuiwezesha Qatar kupata wafanyakazi wenye ujuzi, uzoefu na nidhamu kwa maslahi ya pande zote mbili.
Katika tukio jingine ujumbe wa Tanzania ulitembelea Wizara ya Elimu na Elimu ya Juu ya Qatar na kufanya mazungumzo na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhe. Ibrahim bin Saleh Al Nuaimi ambapo pamoja na mambo mengine, walijadiliana namna ya kuimarisha ushirikiano katika sekta ya elimu na kubadilishana wakufunzi na walimu wa ngazi mbalimbali.
Ujumbe wa Tanzania pia ulitembelea Kampuni ya Usafirishaji ya MOWASALAT na kujadiliana namna kampuni hiyo inavyoweza kuendelea kuwaajiri Watanzania wengi zaidi na kujifunza namna inavyoendesha shughuli zake za usafirishaji nchini humo. Kampuni ya MOWASALAT imeajiri zaidi ya Watanzania 160 ambao wapo nchini Qatar kwa sasa.