Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la usimamizi wa mazingira na maendeleo Tanzania (EMEDO),Editrudith Lukanga akizungumza na waandishi wa habari mkoani Arusha.
Baadhi ya Wafanyabiashara wa samaki na dagaa wakiendelea na biashara zao jijini Arusha .
……………………………..
Julieth Laizer ,Arusha.
Serikali imeombwa kuwatambua wanawake walioko katika sekta ya uvuvi kwa kuwapatia mitaji mikubwa sambamba na kuwaboreshea miundombinu ili waweze kuondokana na changamoto mbalimbali.
Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la usimamizi wa mazingira na maendeleo Tanzania (EMEDO) ,Editrudith Lukanga wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani Arusha.
Lukanga amesema kuwa,wanawake katika sekta ya uvuvi wanafanya vizuri ,ila bado kuna changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo ikiwemo kutokuwa na mitaji ya kutosha kwa ajili ya kuendesha shughuli zao.
“Kwa kweli wanawake wanafanya vizuri sana katika sekta ya uvuvi ila changamoto kubwa ni mitaji mikubwa kwa ajili ya kukuza na kuendeleza biashara zao kwani wengi wao wana uwezo mkubwa wa kufanya biashara hizo ila changamoto ni mitaji ,hivyo naomba sana serikali iweze kuangalia katika jicho la kipekee ili kusaidia wanawake hao.”amesema Lukanga.
Amesema kuwa, shirika hilo limekuwa likiwasaidia wanawake waliopo katika vikundi ambapo linalenga katika kuimarisha uwezo wa jamii ili kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo na hasa katika kutumia ,kulinda na kuhifadhi mazingira na maliasili kwa ajili ya kuboresha maisha.
Ameongeza kuwa, shirika hilo limejikita kuimarisha uwezo wa jamii katika kutunza mazingira na kupambana na umaskini, kupitia mafunzo,utafiti ,uchanganuzi wa sera, ushawishi na utetezi,uhamasishaji ,kupeana taarifa pamoja na uhusiano wa kitaasisi na utafutaji wa rasilimali.
Lukanga ameongeza kuwa,shirika hilo la EMEDO kwa kushirikiana na shirika la Umoja wa mataifa la chakula na kilimo duniani(FAO) pamoja na wizara ya mifugo na uvuvi inatekeleza mradi unaolenga kuwawezesha wanawake katika uvuvi mdogo nchini Tanzania.
Amesema kuwa, mpango huo unachangia katika utekelezaji wa kanuni za miongozo ya hiari ya kuhakikisha kuwa uvuvi mdogo unakuwa endelevu kwa muktadha wa usalama wa chakula na kuondoa umaskini.
Amefafanua kuwa,mradi huo unatekelezwa katika ukanda wa Ziwa Victoria na utawanufaisha wanawake wachakataji na wafanyabiashara wa samaki kupitia jukwaa lao la kitaifa ambalo linaitwa TAWFA lengo likiwa ni kujenga na kuimarisha msingi wa taasisi hiyo katika ngazi ya wilaya,mikoa na hatimaye kanda ya ziwa Viktoria .
Ameongeza kuwa, utekelezaji wa mradi huo unafanyika katika muktadha wa mwaka wa kimataifa wa uvuvi wa mdogo na ufugaji wa viumbe majini (IYAFA 2022) na hivyo kutoa fursa kwa wanawake wachakataji na wafanyabiashara wa samaki na mazao yake kuweza kuelewa juu ya malengo na misingi ya mwaka huu muhimu kwao.