**********************
Nasema hakuna, ni sawa na mama kwa mwanaye, hawezi kuyafuta mema ya mzazi wake, wala chochote juu yake.
Kitendo cha kumlea tangu akiwa tumboni, kumnyonyesha na kumfundisha lugha miaka miwili, akakua na kuufahamu Ulimwengu hakiwezi kufananishwa na chochote duniani.
Hata kama mama huyo atampiga na kumtusi vipi mwanaye lakini bado kosa lake haliwezi kufuta wema aliomfanyia.
Hivyo hivyo kwa Paul Makonda ambaye leo hii ni Mkuu wa Mkoa, huyu amepigana vita kubwa kubwa zilizowashinda wengi, vita za Makonda ni sawa kama zile za Goliathi aliyetajwa katika Biblia, Masalakulangwa na Jing’weng’we waliotajwa katika simulizi za kale.
Makonda naye amesambaratisha makundi mbalimbali likiwemo maarufu kama kundi la Mafia la wauza madawa ya kulevya yalioangamiza vijana wa kitanzania na wengine kufungwa jela huko nje ya nchi, mfano nchini China, zaidi ya vijana takribani 200 walishitakiwa na wengine wamefungwa jela, nchini Brazil vijana wasiopungua 200 walishitakiwa na wengine wamefungwa jela, Afrika Kusini vijana wasiopungua 200 walishitakiwa kwa makosa ya biashara haramu na wengine wamefungwa jela, achilia mbali nchi nyingine na waliongamia na kushitakiwa hapa hapa nchini kwa sababu ya biashara hii haramu.
Jana, vyombo vya habari vimeripoti kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam amesaidia watoto 60, wanaotoka familia masikini ktk Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).
Mkurugenzi mwendeshaji katika kitengo cha Moyo Profesa Mohamed Janabi amesema mapaka sasa watoto 30 kati ya 60 wamefanyiwa upasuaji ndani ya miezi mitatu na kadiri siku zinavyokwenda imeripotiwa kwamba, hadi sasa kuna zaidi ya watoto 500 wenye tatizo la moyo lakini wazazi hawana uwezo wa kumudu gharama za matibabu.
Pamoja na ripoti hiyo ya taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete imemshukuru Mkuu wa Mkoa Paul Makonda kwa kuwajali watoto hao ambao anawalipia kila awamu watoto kumi 10.
Mkuu wa Mkoa Paul Makonda ameishukuru taasisi hiyo ya Moyo ya Jakaya Kikwete na vile vile ameishukuru Wizara ya Afya chini ya Waziri Mhe. Ummy Mwalimu kupitia Serikali chini ya Uongozi wa Rais Dk. Magufuli kwa fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya matibabu kama hayo na kuongeza kuwa, anamshukuru Balozi wa Jumuiya wa Falme za Kiarabu kwa kumuunga mkono na kwa kuleta Madaktari Bingwa kutoka nje ya Nchi ili kuja kufanya upasuaji wa watoto hao wanaotoka familia duni za kimasikani.
Sambamba na hilo, Mkuu wa Mkoa Ndg. Paul Makonda amesema kwamba, mwezi wa 11 hadi wa 12 mwaka huu utakuwa mwezi wa kushukuru wananchi wa Dar es Salaam kwa namna wanavyotoa ushirikiano mbalimbali kwa serikali katika mkoa.
Lengo kuu la tukio hilo ni kufanikisha upatikanaji wa fedha bilioni moja itakayokusanywa kutoka taasisi za kibenki, makampuni na wadau mbalimbali ili fedha hizo zikagharimie matibabu ya watoto hao.
Lakini pia, ameongeza kuwa, anatamani sana kuona watoto hao wanafurahi pamoja na jamii katika siku kuu mbalimbali zinazowakutanisha watu na kufurahi.
Akiongea mbele ya waandishi wa habari, Makonda alikusia juu ya maswali mbalimbali yanayoulizwa na baadhi ya watu wanaohoji ni wapi Mkuu Makonda anapata fedha za kugharamia matibabu ya watoto na misaada mbalimbali anayoitoa kwa wahitaji/watu masikini?
RC. Makonda amesema ya kwamba, “Nchi hii ni tajiri na watu wa nchi hii ni matajiri, wanachohitaji ni mtu mwaminifu, mwadilifu anayeomba fedha kwa matumizi sahihi.”
Sasa nauliza, Mungu awape nini watanzania ikiwa vijana kama huyu Makonda wanafanya mambo makubwa ya kitume katika taifa hili?
Kuna kosa gani laweza kufuta wema anaoufanya Paul Makonda kwa watanzania?
Mimi nafikiri kama kuna jambo la kufanya ni watanzania kumuombea Makonda ktk njia zake na kumuomba pia Rais wa nchi Dk. John Magufuli ampe kiti/dhamanaa kubwa zaidi ya hapo alipo huyu “Paul Makonda” ili apate nguvu ya kuhudumia taifa zima akiwa kiongozi wa kitaifa. Hii ni kwa sababu, anayoyafanya Makonda si ya Mkuu wa Mkoa, kimkoa pekee, bali ni zaidi ya Mkoa.
Tumepata Rais mzuri, na tunapata vijana wazuri sana katika taifa letu, ni muhimu sana kuwashikilia kwa mikono miwili maana bahati haiji mara mbili mbili.