Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha
Baadhi ya maeneo Halmashauri ya Mji Kibaha, Mkoani Pwani yanakabiliwa na kero ya Ukosefu wa maji ya uhakika kwa takriban mwezi mmoja Sasa hali inayosababisha kero kwa wananchi.
Kutokana na kero hiyo ,Baraza la madiwani Kibaha Mjini , limeitaka Mamlaka ya maji na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA )kuweka mipango ya muda mrefu kutatua kero hiyo inayojirudia Mara kwa Mara.
Akiuliza swali la papo kwa papo na kulielekeza Taasisi ya maji DAWASA katika Baraza la madiwani Kibaha Mjini ,diwani wa kata ya Mbwate ,Fokas Bundala alieleza ,wanapata tabu ya upatikanaji wa maji ya uhakika ,kwa muda mrefu sasa bila kuwa na majibu ya kina.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha ambae pia ni Diwani wa Sofu Mussa Ndomba alieleza ,inasikitisha chanzo Cha Ruvu na Mlandizi Vipo Kibaha ,Pwani Lakini maji hayapatikani kwa uhakika huku Dar es Salaam wakipata maji.
“Tunasubiria maji usiku, unakuta mtu anaangalia kipindi cha TV hata kama hapendi kuangalia ili asubirie maji, chanzo kipo kwetu ,Lakini tunapata maji kwa shida kama tupo pembezoni mwa mji kumbe Mjini,na tatizo hili limekuwa la kujirudia”alifafanua Ndomba.
Nae Diwani wa Visiga, Kambi Legeza alitaja kero nyingine, ni wateja waliolipia vifaa na kuunganishiwa maji kushindwa kufikishiwa huduma kipindi kirefu takriban mwaka mzima sasa .
“Wateja wengi wamelipia lakini tatizo vifaa,je ofisi yenu DAWASA inakwama wapi,alihoji Kambi.
Hata hivyo Kambi ,alitaka pia DAWASA kuangalia namna ya kupunguza mzigo kwa miradi ya RUWASA ambapo wananchi wanalipia mara tatu huku DAWASA ikitakiwa kuipokea baada ya ujenzi.
Diwani viti maalum Kibaha Mjini,Selina Wilson aliitaka DAWASA kusimamia tatizo linalodaiwa na baadhi ya wananchi kulalamikia kubambikiwa bill suala ambalo linaondoa uaminifu .
Vilevile, kushughulikia mafundi vishoka na mafundi ambao wameshawaondoa kazini wajulikane na wasiendelee kupita kwa wateja na kutumia mwamvuli Kuwa bado watumishi.
Akitolea ufafanuzi juu ya kero hizo ,kutoka DAWASA Kibaha upande wa miradi Mhandisi Yohana Msangula alikiri kuwa tatizo lipo na kusema uzalishaji ni mdogo kutokana na tatizo la umeme.
Alisema ,Shirika la Umeme TANESCO lipo kwenye matengenezo ya muda mfupi na watakapokamilisha tatizo linaisha.
Akielezea suala la wateja ambao wameshalipia vifaa kutounganishiwa huduma ya maji kwa wakati , Yohana alieleza ,maombi ya wateja ni mengi ,muitiko mkubwa tofauti na lengo lao hivyo wamejipanga kuanza na wateja ambao wamelipia tangu mwezi Mei mwaka huu na baadae wataendelea na wateja wapya.
Kuhusu , tatizo la maji shule ya Sekondari Viziwaziwa , Pichandege na Msangani alisema kwamba, wanafanya marekebisho kwenye miradi maeneo yenye uhitaji wa kurekebishwa na kutengeneza na kuboresha miundombinu awamu kwa awamu kulingana na miradi lengwa.