Mratibu wa mafunzo Salum Danford kutoka SIDO akitoa elimu kwa wajasiriamali juu ya matumizi sahihi ya fedha za mikopo wanazoziomba kwaajili ya kuendeleza biashara zao
Wajasiriamali kutoka Wilaya mbalimbali za Mkoa wa Mwanza wakiwa kwenye mafunzo
…………………………………………
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Shirika la kuendeleza Viwanda vidogo (SIDO) Mkoani Mwanza limetoa mafunzo kwa wajasiriamali 48 juu ya kutumia vyema mikopo waliyoomba kwaajili ya kuendeleza biashara zao.
Mafunzo hayo yalifanyika jana Jumatano Agositi 24,2022 kwenye ukumbi wa mikutano wa SIDO Mkoani hapa.
Salum Danford, ni mratibu wa mafunzo hayo alisema lengo kubwa la mafunzo hayo ni kuwapa elimu wajasiriamali wanaojishughulisha na uzalishaji wa biashara mbalimbali kuzitumia vizuri fedha wanazoziomba za mikopo ili ziweze kuwasaidia kupanua biashara.
Alisema pamoja na kuwapa elimu ya kutumia fedha hizo vizuri pia wanawaasa kuwa warejeshaji wazuri kwa kufuata taratibu na sheria zilizowekwa za mikopo ili kuweza kutunisha mfuko na wengine waweze kukopa.
Danford alisema wameshusa riba kutoka asilimia 18 hadi asilimia 9 ili kuweza kuwasaidia wajasiriamali kumudu gharama za marejesho na kufanya biashara zao kwa amani.
Aliongeza kuwa kutokana na mafunzo waliyowapa wajasiriamali hao wanaimani watafika mbali katika kukuza biashara zao.
Alieleza kuwa wajasiriamali hao waliomba mikopo katika Shirika la SIDO na Shirika limewapitishia milioni 107 ili ziweze kuwasaidia katika kukuza na kuendeleaza biashara zao.
Kwaupande wake Consolata Gecha, mjasiriamali kutoka Wilaya ya Misungwi anaejihusiha na ushonaji wa nguo za maharusi alisema elimu aliyoipata itamsaidia kuendesha biashara yake kwa ufanisi mkubwa.
Naye Gerald Zacharia, majasiriamali anaejihusiha na ufugaji wa kuku alisema SIDO imemsaidia kupanua wigo wa biashara yake kwa kumpa elimu na mkopo.