**********************
Namwandishi wetu.
Pamoja na kuwa chanzo cha takwimu kwa ajili ya maendeleo ya Tanzania, Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 ina vipengele mahsusi vinavyolenga Sekta ya Mawasiliano na matumizi ya huduma zinazotolewa.
Pamoja na shughuli nzima ya sensa kufanikishwa na matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano, karibu asilimia 28 ya maswali kwa wananchi yanahusiana ama moja kwa moja au kwa namna nyingine na masuala ya mawasiliano; sekta wezeshi, ambayo imechangia katika kukua kwa maeneo mengine ya kiuchumi na kijamii Tanzania.
Maswali hayo yamegusia vipengele muhimu katika mawasiliano; ambavyo ni uwepo wa huduma husika, kuenea kwake, upatikanaji, kuchukuliwa kwa matumizi, matumizi yenyewe, aina ya matumizi na watumiaji. Hivi vinatumika kama vipimo vya maendeleo ya sekta katika jamii yoyote, siyo hapa nchinitum bali duniani kote.
Kuna swali kuhusu umiliki wa simu na vifaa vya mawasiliano. Aidha, anayehojiwa anatakiwa kutaja namba yake ya simu ya mkononi. Lengo ni kuwa na kanzidata ya watumiaji. Kwa bahati mbaya hakuna swali kuhusu simu za mezani, labda kwa kuwa matumizi yake kwenye makazi yameshuka sana miaka ya karibuni.
Majibu ya maswali kuhusu ulemavu yatasadia kuandaa mipango endelevu kwa makundi mbalimbali ya watu wenye ulemavu kulingana na mahitaji yao kwenye mawasiliano, hasa kujua aina ya vifaa saidizi wanavyohitaji, kama vile simu zenye sauti kubwa, mitetemo maalum na programu tumizi zinazowezesha watumiaji wenye changamoto mbalimbali kuwasiliana kwa urahisi.
Kwa Tanzania, huduma za mawasiliano ni pamoja na simu za mkononi na mezani, intaneti, utangazaji,posta na usafirishaji wa vifurushi na huduma zinazowezesha na matumizi haya. Mojawapo ya huduma hizo ni huduma za fedha kupitia simu za mkononi na huduma za mawasiliano mtandaoni ikiwa ni pamoja na mikutano na kupata matangazo ya televisheni na redio.
Taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imebainisha kwamba hadi Juni 2022, kulikuwa na laini za simu za mkononi 56.3 milioni. Simu za mkononi zimeenea kwa asilimia 94 na matumizi yake kufanya miamala mbalimbali yamewezesha watanzania wengi kujumuika katika mfumo wa kifedha.
Mkrugenzi Mkuu wa TCRA, Dkt. Jabiri K. Bakari anasema, Pamoja na faida kwa watumiaji, wakala na taasisi za kifedha huduma za fedha kupitia simu za mkononi zimeiwezesha Tanzania kuwa nchi ya kwanza ulimwenguni kuwa na mfumo kamili uliowezesha muingiliano wa mitandao ya fedha kupitia simu za mkononi.
Kuenea kwa matumizi ya simu kwa miamala ya kifedha kumekwenda sambamba na kukua kwa matumizi ya simu za mkononi. Akaunti za pesa kupitia simu zimekuwa kwa kasi. Taarifa ya mwaka 2019/2020 ya Benki Kuu ya Tanzania inaonyesha kwamba miamala ya kifedha kupitia simu za mkononi imekua kwa asilimia 21.8 kwa ukubwa na asilimia 8.9 kwa thamani ya miamala ukilinganisha na 2018/2019
Kimsingi, ukusanyaji wa takwimu una lengo la kuwezesha mipango ya Taifa kwa lengo ka kuboresha Maisha ya watu, kufanya uamuzi wenye ushahidi, kujua hali ya wananchi na uchumi kwa ujumla, kupata nyenzo za kutatulia matatizo ya maendeleo na kuhakiki utekelezaji wa malengo ya Kitaifa ya kimkakati.
Vilevile takwimu zinaiwezesha serikali kulinganisha mipango yake na raslimali zilizoko, kujua mahitaji ya wananchi, kupitia upya mipango na mikakati kwa malengo ya kuiboresha na kutumia raslimali kwa njia endelevu.
Tanzania inatelekeza mpango wa kujenga uchumi wa kidijitali, ku imarisha mawasiliano vijijini na kupunguza gharama za uendeshaji serikali na kuifanya kuwa kitovu cha biashara mtandao Afrika ya Mashariki na miongoni mwa nchi wanachama wa Umoja wa Ushirikiano Kusini mwa Afrika (SADC). Haya yanahitaji takwimu sahihi za mawasiliano ili kuwezesha huduma zinazotarajiwa na kufikia malengo.
Takwimu ni muhimu wa watoa huduma kuchambua idadi ya watu, mahali walipo, umri wao, elimu zao na shughuli zao za kujikimu na kuandaa mikakati ya kuwafikia na kuendelea kuwahudumia.
Kwa mfano, majibu kuhusu mahali alipo anayehojiwa, jinsia, ulemavu, viwango vya elimu na shughuli za kila siku yanaweza kutumika katika kuanda mikakati ya kuondoa tofauti za matumizi kijinsia, kijiografia, kiuchumi, uelewa na uwezo wa kutumia.
Kuna aina tatu za tofauti katika kupata na kutumia huduma za mawasiliano; ambazo ni tofauti ya matumizi kati ya wanawake na wanaume; kati ya watumiaji mijini na vijijini, uwezo wa kumudu vifaa vya mawasiliano na gharama za matumizi na uelewa.
Tofauti hizi zikichambuliwa vinaonyesha tofauti nyingine – kwa mfano kunaqeza kuwa na tofauti miongoni mwa wanaume au wanawake kwa kuzingatia walipo; yaani mijini au vijijini, kwa kipato, ulemavu, uwezo wa kumudu gharama, na kadhalika.
Taarifa ya mwaka 2021 ya Umoja wa Maendeleo wa nchi 37 za Ulaya, unaojulikana kwa kufupi chake kama OECD unaonyesha kwamba tofauti za kupatikana kwa matumizi, kumudu gharama vimechangia katika kuongeza tofauti za matumizi kijinsia. Inasema wanawake wako nyuma katika kumilki na kutumia simu za mkononi.
Taarifa hiyo inapendekeza kuwepo mipango ya kuendelea wanawake kielimu na kuwashirikisha katika uchumi na siasa ili wawe sehemu ya ukuaji wa jumla wa jamii walipo.
Taarifa inapendekeza kuimarishwa kwa mfumo wa kukusanya takwimu ili kuwezesha kufanyika maamuzi endelevu. Upatikanaji wa takwimu na wadau wote kuzitumia kwa pamoja kuharakisha uondoaji wa tofauti zilizoko katika upatikanaji na matumizi ya huduma za mawasiliano.
Masuala mengi ya kimaendeleo yanachangia katika kukua kwa matumizi ya mawasiliano. Kwa mfano, kupatikana kwa umeme vijijini ni muhimu katika kuendeleza uwekezaji na matumizi. Kuendeleza mila na desturi zinazomnyima mwanamke fursa ya kujiamulia masuala yake ya kimsingi ikiwemo kujitafutia kipato kunakwamisha uweekano wake wa kumilki na kutumia vyombo vya mawasiliano.
Tanzania inatekeleza mipango kadhaa kuondoa tofauti hizi. Mojawapo ni kuanzishwa kwa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, kwa kifupi UCSAF, ambao ulianzishwa mwaka 2006 na kuanza kazi 2009 kuratibu ruzuku kwa watoa huduma kufikisha huduma za mawasiliano kwenye maeneo ambayo sio rahisi kufikika.
Serikali imepanga kufikisha huduma za TEHAMA kwa vijiji 718 aambavyo hadi sasa havijaunganishwa na mitandao ifikapo mwaka 2025, kwa mujibu wa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape M. Nnauye.