**************************
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kuimarisha ulinzi na usalama kwa kufanya operesheni, misako na doria mbalimbali hali inayopelekea amani na utulivu kwa raia na mali zao ndani ya Mkoa wetu.
Mtakumbuka mnamo tarehe 16.08.2022 majira ya saa 03:00 asubuhi huko maeneo ya Inyala Pipeline, Kijiji cha Shamwengo, Kata ya Inyala, Tarafa ya Tembela, Wilaya ya Mbeya Vijijini katika barabara ya Mbeya – Njombe ilitokea ajali mbaya iliyohusisha magari manne na kusababisha vifo vya watu 19 na majeruhi zaidi ya ishirini.
Baada ya ajali hiyo dereva wa Gari lori lenye namba za usajili T.387 DFJ / T.918 DFE aina ya Dayun mali ya kampuni ya Evarest French Ltd likiwa limebeba kontena la mchanga likitokea Mbeya kuelekea Dar es Salaam alikimbia.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilianza ufuatiliaji na mnamo tarehe 20.08.2022 mtuhumiwa aitwaye MUKSIN MGAZA GUMBO [24] Dereva wa Lori na Mkazi wa Dar es Salaam alikamatwa huko eneo la Mabibo Jijini Dar es Salaam kuhusiana na kusababisha ajali iliyopelekea vifo na majeruhi.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea na mahojiano na mtuhumiwa na mara baada ya upelelezi kukamilika atafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria. Nitoe rai kwa madereva kuwa makini wawapo barabarani sambamba na kujenga tabia ya kufanya ukaguzi wa vyombo vyao vya moto mara kwa mara ili kuhakikisha kabla ya kuanza safari vipo katika hali nzuri.
ASHIKILIWA NA JESHI LA POLISI KWA KUTOFIKA KITUO CHA SENSA KWA KUSINGIZIA UGONGWA.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia Karani wa Sensa Kata ya Ilomba Jijini Mbeya LUTENGANO MWAKIBAMBO kwa tuhuma za kutofika kituo chake cha sensa kwa kusingizia ugongwa.
Ni kwamba mtuhumiwa baada ya kulipwa fedha taslimu shilingi 600,000/= kama malipo ya awali alitoweka na mnamo tarehe 21.08.2022 baada ya kusikia malipo ya awamu ya pili yanatolewa alirudi tena kwa ajili ya kusaini fedha hizo ndipo alikamatwa. Mtuhumiwa anaendelea kuhojiwa na mara baada ya upelelezi kukamilika atatendewa kwa mujibu wa sheria.