Mkuu wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, Edward Mpogolo (kulia) akijumuika kupata kahawa na wananchi wa Kata ya Irisya ikiwa ni njia ya kujua changamoto zao baada ya kufanya mkutano wa hadhara katika kata hiyo jana.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, Edward Mpogolo (wa pili kulia) akijumuika kupata kahawa na wananchi wa Kata ya Irisya ikiwa ni njia ya kujua changamoto zao baada ya kufanya mkutano wa hadhara katika kata hiyo jana. Kulia ni Afisa Mipango wa wilaya hiyo, Thomas Mwailafu ambaye alimwakilisha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi.
Mzee Ramadhani Athumani akizungumzia tukio la Mkuu huyo wa wilaya kwa kutembelea wananchi katika vijiwe vya kahawa.
Mzee Ismail Nkungu (90) akiongelea tukio hilo.
Omari Shabani akizungumzia tukio hilo na kumuomba Rais Dkt. John Magufulia amuongezee cheo.
Na Dotto Mwaibale, Singida
MKUU wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, Edward Mpogolo amewashangaza wananchi wa Kata ya Irisya pale alipoamua kulala katika kata hiyo na kwenda kwenye vijiwe vya wauza kahawa na tangawizi kujua changamoto zinazo wakabili wananchi.
Tukio hilo limeelezwa na wananchi wa kata hiyo kuwa halijawahi kutokea na wala kuliona tangu kuanzishwa kwa kata hiyo na kuwa linapaswa kuigwa na viongozi wengine ili kuharakisha maendeleo ya wananchi.
Mpogoro alifanya tukio hilo kwa nyakati tofauti juzi na jana baada ya kufanya mikutano ya hadhara wakati akiwa kwenye ziara ya kazi ya kujua changamoto za wananchi na kujitambulisha kwao baada ya Rais Dkt. John Magufuli kumteua kuongoza wilaya hiyo.
Akizungumzia tukio hilo Mzee Ramadhani Athumani amesema hajawahi kuona jambo la namna tangu kuanzishwa na kuwepo kwa kata hiyo.
” Kwa kweli tukio alilofanya DC huyu kwetu ni la kihistoria kwani halijawahi kutokea na linapaswa kuigwa na viongozi wengine kwa kuwa linamsaidia kujua changamoto za wananchi ambao hawakuwepo kwenye mikutano yake ya hadhara” alisema Athumani.
Athumani alisema kuwa pia tukio hilo linamfanya DC huyo kuwa jirani zaidi na wananchi badala ya kuogopwa.
Mzee Ismail Nkungu (70) alisema tangu azaliwe hajawai kumuona kiongozi wa namna hiyo kwani viongozi wote wanaofika katika kata hiyo huwa wanakuwepo kwa muda wa masaa mawili au matatu na kuondoka.
Omari Shabani yeye alisema kuwa DC huyo ni wa mfano kwani kwa kipindi kifupi alimbacho yupo katika wilaya hiyo tangu ateuliwe ameonesha kuwa ni mchapa kazi hivyo amemuomba Rais amuongezee cheo lakini asihamishwe kwenye mkoa huo ili aendelee kuwatumikia wananchi.
” Mpogolo ni mkuu wa wilaya wa haina yake kaja kukaa na sisi kwenye hivi vijiwe vya kahawa na kuja kulala maeneo haya ambayo hayana hata umeme kweli huyu ndiye kiongozi tunaye mtaka.
Muuza kahawa wa moja ya kijiwe cha kahawa katika kata hiyo Seleman Shabani alisema hakika DC huyo ni mtu wa watu na tangu aanze kufanya biashara hiyo hajawai kuliona tukio la namna hiyo.
Shabani amesema kwao wauza kahawa ujio wa DC huyo imekuwa fursa kwani licha ya kuzungumza na wananchi pia aliwanunulia kahawa zaidi ya watu 200.
“Tangu nianze kufanya biashara hii sijawahi kuuza kahawa kwa kiasi hiki kwa siku moja kwani nimelazimika kupika kahawa mara nne kutokana na wingi wa watu waliofika kuzungumza na DC usiku huu” alisema Shabani.
Mpogolo alikuwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo na kuzungumza na wananchi ili kujua changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi ambapo alitembelea kata tatu za Sepuka, Irisya na Mwaru zenye jumla ya vijiji 11.