Marehemu Winjuka Songalaeli Mkumbo enzi za uhai wake.
Madiwa hao wakiwa tayari kwa ajili ya ibada hiyo iliyoongozwa na Askofu wa Kanisa la Assemblies of God Singida Kaskazini, Noel Lameck.
Askofu Noel Lameck akiongoza ibada hiyo.
Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dorothy Mwaluko, akitoa salama za rambirambi za mkoa.
Na Dotto Mwaibale, Singida
AJALI ya Basi la Tanzanite lenye namba za usajili T 916 DNU iliyoua watu tano mkoani
Singida imeibua mapya baada ya mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo kueleza kuwa
mabasi yanayofanya safari kati ya Mwanza, Dodoma na Dar es Salaam madereva
wamekuwa wakishindana kufika mapema kwa kuchochewa na bonasi inayotolewa na matajiri wa
magari hayo.
Hayo yalibainishwa na Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara Wanawake Mkoa
wa Singida, Prisca Maleta anayeishi Manyoni mkoani hapa ambaye alikuwa mtu wa
kwanza kushuhudia ajali hiyo na kutoa msaada kwa majeruhu na kuzistiri maiti.
Maleta aliyasema hayo jana kwenye ibada ya mazishi ya Diwani Viti Maalum wa
Tarafa ya Kinampanda Wilaya ya Iramba Winjuka Mkumbo ambaye alikuwa ni
miongoni ya watu waliopoteza maisha katika ajali hiyo.
“Mimi ni Mwanaharakati nilifuatilia jambo ili na nilipoongea na
Winjuka eneo la ajali aliniaambia mwendo wa basi hilo tangu linaondoka Singida
ulikuwa mbaya kwani dereva alikuwa akiendesha kwa kasi na kusababisha abiria
kuanza kutafutana na walipofika Manyoni abiria walimkataa na akaanza kuendesha
dereva mwingine wa akiba ambaye naye alikuwa akiendesha kwa mwendo wa kasi
kuliko yule wa mwanzo hadi tairi lilipopasuka na kusababisha ajali”
alisema Maleta.
Alisema alipofuatilia kwa karibu aligundua sababu ya mwendo kasi wa mabasi
hayo ni madereva hasa wa mabasi ya kutoka Mwanza kugombea mnara yaani anayekuwa
wa kwanza kufika anapewa bonasi na matajiri wa mabasi hayo.
“Tunaomba Serikali kuliangalia jambo ili kwani matajiri wengi
wanawapatia madereva wao minara na wa kwanza kufika ndiye atakayepewa bonasi na
suala la pili ni wale watu wanaofika
eneo la ajali tukiwaamini kwa asilimia 100 ndio wanakuwa wa kwanza kuwafilisi
kwa kuwaibia majeruhi na watu waliopoteza maisha kwani nimewashuhudia kwa macho
yangu na wanangu wakiwafunua zile nguo zetu tulizowa wasitiri kwa kuwafunika na
kuanza kuingiza katika mifuko yao na kuchukua fedha na vitu vingine vya thamani
kwa kuwa tunawafahamu baadhi yao majina tumempa Mwenyekiti wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Manyoni kwa
ajili ya kushughulikia suala hilo” alisema Maleta.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Alhajj Juma Killimbah alisema Rais Samia
Suluhu Hassan ametoa fedha nyingi kwa ajili ya kujenga vituo vya afya, zahanati na Hospitali lengo likiwa ni kuwasaidia wananchi pale wanapokuwa wagonjwa na kupata
ajali lakini amesikitishwa na kitendo cha majeruhi wa ajali hiyo kuona wakipoteza
maisha licha ya kuwepo huduma za hospitali karibu na eneo la ajali.
“Ajali imetokea mlima Saranda, pale Kintinku pana zahanati,Maweni pana
Kituo cha afya na Manyoni pana Hospitali ya wilaya ni umbali wa kilomita
zisizozidi 20 kwa nini hawa majeruhi wasingepelekwa katika maeneo hayo kwa
ajili ya kupata huduma ya kwanza ambayo ingesaidia kuzuia damu zisitoke badala
yake wakawachukua na kuwapeleka Dodoma umbali wa zaidi ya kilometa 150 bila usaidizi wowote na baadhi
yao kujikuta wakipoteza maisha akiwepo diwani Winjuka” alisema Killimbah.
Killimbah alitumia nafasi hiyo kutoa agizo kwa Serikali kuhakikisha
inaaliangalia jambo hilo kwa karibu na kuwa itakuwa haina maana kuwa na
zahanati, vituo vya afya, hospitali kila mahali lakini wananchi wanapoteza
maisha kwa kuwasafirisha umbali mrefu kwa ajili ya kuwapatia matibabu huku
wakikosa huduma kwenye maeneo ya karibu ambazo
zingesaidia kuokoa maisha yao.
Katika mazishi hayo simanzi na vilio na watu kuzimia vilitawala huku kila
mtu akimzungumzia marehemu Winjuka Mkumbo kwa jinsi alivyokuwa akijitoa
kusaidia jamii katika Wilaya ya Iramba na maeneo mengine ya jirani.
Akiongoza ibada ya mazishi Askofu Noel Lameck wa Kanisa la Tanzania Assemblies
of God Singida Kaskazini alisema umati wa watu uliokuwepo katika ibada hiyo
unaonesha jinsi Winjuka Mkumbo
alivyokuwa akiishi vizuri na jamii na kanisa na akatumia ibada hiyo kumuomba kila mtu
kujiandaa kwa kutubu na kuokoka.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri
ya Wilaya Iramba Michael Matomora akitoa salamu za rambimbia aliagiza kila siku kuhakikisha gari lake
linakuwa limewekwa mafuta ili
kusaidia kusafiri wakati wote hasa kunapokuwepo na jambo la dharura.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Innocent Msengi alisema
halmashauri hiyo tangu itokee ajali hiyo na kumpoteza diwani wao Winjuka Mkumbo
imetoa ushirikiano na kugharamia mambo mbalimbali yaliyokuwa yakihitajika.
Miongoni waliopata fursa ya kumzungumzia marehemu Winjuka ni pamoja na
Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dorothy Mwaluko ambaye alitoa rambirambi kwa
niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mbunge wa Iramba Magharibi ambaye pia ni Waziri wa Fedha na Uchumi , Dk.Mwigulu
Nchemba, Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa
wa Singida, Martha Gwau, Wajumbe wa Kamati ya Siasa kutoka wilaya ya Iramba na
Mkoa wa Singida wakiwepo, Diana Chilolo, Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa, Ahmed
Kaburu.
Makundi mengine yaliyopata fursa ya kutoa rambirambi zao na kumzungumzia
marehemu Winjuka ni vikundi vya wananawake vilivyokuwa vikisaidiwa na marehemu,
wanafunzi zaidi ya 900 waliokuwa wakisomeshwa na kusaidiwa na marehemu kupitia
Shirika la Ndugu la Sweden, watu binafsi, makanisa mbalimbali na taasisi
zingine zilizopo wilayani humo.
Marehemu Winjuka Songalieli Mkumbo alizaliwa tarehe Oktoba 6, 1974 katika
Kijiji cha Simbalugwala ambapo alihitimu darasa la saba mwaka 1989 na kufunga
ndoa na John Lyanga katika Kanisa la T.A.G Mwaka 1991.
Enzi za uhai wake marehemu ameshika nyazifa mbalimbali katika kanisa na
maeneo mengine na hadi anafariki alikuwa Diwani wa Viti Maalum wa Tarafa ya
Kinampanda wilayani Iramba mkoani Singida.
Marehemu Winjuka Mkumbo alifariki Agosti 17, 2022 kwa ajili ya gari
iliyotekea Mlima Saranda wilayani Manyoni na ameacha mme, watoto watatu, wawili wa
kike na wakiume mmoja Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi amen.