******************
Na Joseph Lyimo
Wadau mbalimbali wa maendeleo wa Mkoa wa Manyara, wameiasa jamii kuhakikisha kuwa wanaendelea kupata chanjo ya UVIKO-19 kwani janga hilo bado lipo na lina madhara kwa jamii.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wadau hao wanadai kwamba janga la janga la UVIKO-19 bado lipo hivyo jamii inapaswa kushiriki kujikinga kwa kupata chanjo ya UVIKO-19.
Mkazi wa mtaa wa Nyungu Mjini Babati, Abdilahi Ismail anaeleza kuwa jamii isibweteke kutokana na kutokuwepo na mlipuko wa UVIKO-19 hivyo waendelee kushiriki kupata chanjo ya UVIKO-19.
Ismail anaeleza kwamba pamoja na hayo jamii ihakikishe inashiriki chanjo ya UVIKO-19 ambayo Serikali kupitia wataalam wa afya katika vituo mbalimbali vilivyotengwa.
“Janga la UVIKO-19 bado lipo nchini hivyo wananchi kwa ujumla wao wanapaswa kushiriki kupatiwa chanjo kwa wale ambao bado hawajachanja hadi hivi sasa,” anasema Ismail.
Mkazi wa kata ya Bagara, Christopher Bayo anaeleza kwamba yeye binafsi ameshapata chanjo ya UVIKO-19 ila anawaasa wananchi ambao hawajapata chanjo hiyo wahakikishe wanapata.
“Watu wanatakiwa kutambua kuwa janga la UVIKO-19 bado lipo hivyo hakuna sababu yoyote ya kutoshiriki kupatiwa chanjo ya janga hilo la UVIKO-19 ambalo bado lipo.
Mratibu wa shirika lisilo la kiserikali la Saidia Wanajamii Tanzania (SAWATA) lenye makao makuu yake Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro, Mohamed Issa Mughanja anasema jamii inapaswa kushiriki kupata chanjo hiyo kwani UVIKO-19 bado ipo.
“Bado changamoto ya janga la UVIKO-19 ipo hivyo wananchi washiriki kupata chanjo hiyo kwani viongozi wa serikali kupitia wataalam wa afya wanatoa elimu kila siku juu ya chanjo hiyo,” anasema Mughanja.
Anaeleza kuwa yeye binafsi ameshapatiwa chanjo ya UVIKO-19 na hakuona madhara yoyote hivyo wananshi wanatakiwa kushiriki kupata chanjo hiyo ambayo inatolewa na wataalam wa afya.
“Nitoe rai kwa wachimbaji wadogo wa madini ya Tanzanite (WanaApolo) kushiriki kupata chanjo hii ya UVIKO-19 kwa mustakabali wa usalama wa afya yetu,” anaeleza Mughanja.
Mbunge mstaafu wa Jimbo la Babati Vijijini, Vrajilal Jituson anasema kwamba jamii inapaswa kupata chanjo ya UVIKO-19 na pia kuendelea kuchukua tahadhari kubwa dhidi ya janga hilo.
Jituson anaeleza kuwa jamii inapasw akuendelea kukaa umbali unaotakiwa (social distancing), kuvaa barakoa, kuna maji kwa sabuni kupitia maji tiririka.
“UVIKO-19 ipo na inasambaa, mimi leo nina wiki nimekutwa na UVIKO-19, ninaendelea na matibabu na dawa, pia tunapaswa kuendelea kutumia dawa zetu za asili,” anasema Jituson.
Mganga mkuu wa mkoa wa Manyara, Dkt Damas Kayera anasema kwamba jamii inaendelea kupatiwa elimu juu ya wao kushiriki kupatiwa chanjo ya UVIKO-19 ili kujilinda na changamoto hiyo.
Dkt Kayera anasema hata hivyo, jamii ya wakazi wa mkoa wa Manyara hivi sasa wanazidi kupata uelewa kwa kufuata maelekezo ya wataalam wa afya, juu ya wao kushiriki kupata chanjo ya UVIKO-19.
“Wananchi wanashiriki kupata chanjo ya UVIKO-19 mara baada ya kutambua kuwa siyo vyema kuendelea kusikiliza maneno ya watu ambao siyo wataalam juu ya kushiriki chanjo hiyo,” anaeleza Dkt Kayera.
Anatoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Manyara, ambao bado hawajapata chanjo ya UVIKO-19 kushiriki vyema kwenye chanjo hiyo kwani shughuli hiyo inatolewa kwenye maeneo mbalimbali.
Anaeleza kwamba wananchi wa Halmashauri saba za Wilaya za mkoa huo za Babati Mji, Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Mbulu Mji, Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Hanang’ na Simanjiro, wanapatiwa chanjo hiyo bila tatizo lolote.
Anasema hatarajii kuona jamii inashindwa kushiriki shughuli ya kupatiwa chanjo ya UVIKO-19 ili hali Serikali imetimiwa wajibu wao kwa jamii kwa kuhakikisha chanjo hiyo inapatikana hadi kwenye ngazi ya kaya.
Mratibu wa uelimishaji na uhamasishaji jamii kutoka Wizara ya Afya, Peter Mabwe anaeleza kuwa malengo ya kitaifa ya utoaji chanjo ni kufikia asilimia 70 ya walengwa wote ambao ni watu wazima kuanzia miaka 18 yatafikiwa ifikapo Desemba mwaka huu.
Mabwe anasema jambo la muhimu ni jamii kuendelea kujitokeza kwa wingi kkuupata chanjo ya UVIKO-19 ili kufikia malengo ya kitaifa ya utoaji chanjo ya ugonjwa huo kwa asilimia 70.
“Serikali inaunga mkono juhudi za wadau wanaojitokeza kuendesha kampeni ya chanjo ya UVIKO-19 na kutoa elimu kwa jamii kwa kuzingatia ainisho la makundi yaliyo katika hatari ya UVIKO-19,” anasema Mabwe.
Anasema kwamba lengo la serikali ni kuhakikisha kuwa nchi inakuwa salama dhidi ya magonjwa na dharura mbalimbali za kiafya na kufikia azma hiyo ni muhimu wananchi wapate taarifa sahihi na kwa wakati.
“Elimu sahihi ni muhimu ili kuepusha upotoshaji unaojitokeza kuhusu UVIKO-19 na dharura nyingine za kiafya ikiwemo wasiwasi wa hatua zinazochukuliiwa kudhibiti magonjwa hayo,” anaeleza Mabwe.
Mratibu huyo anasema lengo ni kufanya hayo ni jamii kuwa salama na kupunguza athari kwenye shughuli za maendeleo na kiuchumi nchini na dunia kwa ujumla, hivyo watanzania wasisite kuchanjwa.
Mlipuko wa kwanza wa UVIKO-19 umetajwa kuanzia kwenye soko la Wuhan nchini China mwaka 2019 na hapa nchini uliingia mwaka 2020, ambapo mgonjwa wa kwanza alipatikana jijini Arusha.
Kwa mujibu wa andiko la chuo kikuu cha Johns Hopkins cha Marekani, watu milioni 550 wamethibitika kupata maambukizi ya UVIKO-19 duniani kote.
Kwa mujibu wa chuo hicho, hadi kufikia mwezi Julai mwaka 2022 zaidi ya watu milioni 6.3 wamefariki dunia kutokana na maambukizi ya UVIKO-19 duniani kote.