*******************
Na Mwamvua Mwinyi, KISARAWE
Agost 21
MJUMBE wa Kamati ya Sensa kitaifa ambae pia ni Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt.Selemani Jafo ametoa Rai kwa Wananchi kutowabughudhi makarani wa sensa na badala yake wawape ushirikiano ili kupata takwimu halisi kwa maendeleo ya Taifa.
Vilevile , ameeleza kamati hiyo imeridhika na maandalizi ya vifaa ,na makarani zaidi ya 200,000 watapita ili kufanikisha shughuli ya sensa itakayofanyika agost 23 Jumanne ya wiki hii.
Akihamasisha wananchi kushiriki kwenye sensa siku hiyo , katika Tamasha la uhamasishaji wa sensa lililoandaliwa na Mkoa wa Pwani, ambalo limefanyika wilayani Kisarawe ,Jafo aliwaasa wananchi kutoa ushirikiano wa kutosha na kuandaa taarifa zao wakati makarani wakifika kuhitaji taarifa.
“Hii ni sensa ya sita ,ambapo ya mwaka huu itakuwa ya aina yake tofauti na zilizopita ,na kutumia teknolojia ya kisasa kurahisisha uhifadhi wa taarifa”:alifafanua Jafo.
Jafo alielezea, wananchi wakae tayari kuhesabiwa agost 23 na Zoezi la kuhesabu madodoso litaendelea kwa siku sita .
Awali Mkuu wa mkoa wa Pwani ,alhaj Abubakari Kunenge alitoa onyo kwa wale watakaofanya uhalifu ama kutaka kuvuruga Zoezi la sensa ,na kusema Serikali ipo macho haijaenda likizo watashughulikiwa kisheria.
Kunenge alisema, sensa ni muhimu kwa maendeleo ya wilaya,mkoa na Taifa kujua takwimu halisi ya watu na makazi.
“1965 sensa ya kwanza na hufanyika kila baada ya miaka 10 ,na sensa zote zilihesabu watu Ila ya mwaka huu ni ya kipekee ambapo watahesabiwa watu na makazi”alieleza Kunenge.
Sambamba na hayo , Kunenge alisema mkoa umefikia asilimia 96 ya maandalizi ya shughuli ya sensa ,mkoa umejiandaa vizuri.
Kwa upande wa wananchi wilayani Kisarawe,Juma Athumani,Heri Dama na Zainab Hassan walisema wamepata elimu ya kutosha na wapo tayari kuhesabiwa kwa manufaa yao na Serikali kijumla .