Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete akitoa maelekezo kwa Mkuu wa Chuo cha Hali ya Hewa, Peter Mlonganile wakati alipokagua maboresho yaliyofanywa kwenye majengo ya chuo hicho Mkoani Kigoma.
Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete akimsikiliza Mkuu wa Chuo cha Hali ya Hewa, Peter Mlonganile kuhusu maboresho yaliyofanyika katika maabara ya Kompyuta, wakati Naibu Waziri huyo alipotembelea Chuo hicho Mkoani Kigoma.
Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete akisisitiza jambo kwa Mkuu wa chuo cha hali ya hewa, Peter Mlonganile (kushoto) kuhusu umuhimu wa Chuo kuwa na vitabu vya kisasa wakati alipotembelea Maktaba ya Chuo hicho ambayo ni sehemu ya maboresho yaliyofanyika chuoni hapo. Wa pili kushoto ni Mbunge wa Kigoma Mjini Kilumbe N’genda na Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Ester Mahawe.
Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete akimsikiliza Mkuu wa chuo cha hali ya hewa, Peter Mlonganile kuhusu matumizi ya vifaa mbalimbali vya maabara wakati Naibu Waziri huuyo alipokagua mradi wa maboresho ya majengo yaliyofanyika katika chuo hicho, Mkoani Kigoma.
PICHA NA WUU
*********************
Naibu Waziri wa Uchukuzi Atupele Mwakibete amemtaka Mkuu wa Chuo cha Hali ya Hewa Tanzania kuhakikisha anabuni mbinu zaidi za kukitangaza chuo hicho ndani na nje ya mipaka ya Tanzania ili kitambulike zaidi na hatimaye kuzalisha wataalam wengi zaidi.
Akizungumza mjini Kigoma baada ya kutembelea Chuo hicho Naibu Waziri Mwakibete amesema wahitimu wa kozi zinazotolewa chuoni hapo ni wa muhimu sana kwani kila sekta inahitaji wataalam wa hali ya hewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi na ushauri kwenye maendeleo mbali mbali ya taasisi za Serikali na binafsi nchini.
“Kozi zinazotolewa hapa ni muhimu sana na zinahitajika kila sehemu lakini taasisi na wananchi bado hawajafahamu uwepo chuo hiki hivyo Mkuu wa Chuo kuwa mbunifu tangaza chuo hiki ili wanafunzi waje wapate elimu na ujuzi’ amesisitiza Naibu Waziri Mwakibete.
Naibu Waziri Mwakibete amempongeza Mkuu wa chuo kwa kuzingatia thamani ya fedha kwenye usimamizi wa mradi wa maboresho ya majengo mbalimbali chuoni hapo ambao umegharimu takribani milioni 400 na kukamilika kwa wakati na viwango.
Naye Mbunge wa Kigoma Mjini Ng’enda ameishukuru Serikali na kusema kuwa maboresho yaliyofanyika yamekifanya chuo kurejea kwenye hadhi yake kwani kabla ya maboresho wakufunzi walilazimika kutumia mabweni kama ofisi hali iliyokuwa ikishusha hadhi ya chuo hasa ikizingatiwa kinadahili wanafunzi wa ndani na nje ya nchi.
Mbunge Ng’enda ameongeza kuwa maboresho makubwa yanayoendelea kufanyika yatakuwa fursa kwa wananchi wa Kigoma kwani yatasababisha kuongezeka kwa kipato cha wananchi hao kwani wananfunzi wanahitaji malazi, vyakula na mahitaji mbalimbali wakiwa masomoni.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho Peter Mlonganile amesema kwa sasa chuo kinatoa kozi chahce ambapo mipango ya mbeleni ni kuendeleza mazungumzo na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Idara ya Fizikia ili kuona namna vyuo hivyo vitakavyoshirikiana kwenye utoaji wa kozi zaidi.
Chuo cha Hali ya Hewa kinamilikiwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ambapo kwa sasa kinatoa kozi za ngazi ya Astashahada ya awali, Astashahada na Stashada za masuala ya hali ya hewa.
(Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikali, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi)