*********************
Na OR-TAMISEMI, Karagwe
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Innocent Bashungwa amewahimiza wananchi kushiriki katika shughuli za maendeleo kwa kujitoa na kuchangia miradi mbalimbali kwenye maeneo yao.
Mhe.Bashungwa ambaye pia ni Mbunge wa Karagwe ametoa rai hiyo Agosti 20,2022 alipokuwa akizungumza kwenye harambee ya kuchangia wa ujenzi wa Kituo cha afya cha Ihembe Wilaya Karagwe mkoani Kagera iliyoandaliwa na wananchi kwa ushirikiano wa uongozi wa kata hiyo.
’’Pamoja na malengo ya Serikali ya kila Tarafa iwe Kituo cha Afya, lakini inapotokea Mwananchi kama nyie wa Kata ya Ihembe mkaamua kuchangia na kuanza kujenga Kituo cha afya, sisi kama Serikali jukumu letu ni kuunga mkono juhudi zenu na kuhakikisha mnakamilisha maelengo yenu,” amesema Mhe.Bashungwa.
Waziri Bashungwa amepongeza wananchi wa Kata hiyo kwa kuonesha mfano na kujitoa kwa michango ya fedha na nguvu kazi ili kuhakikisha wanajenga kituo hicho ambapo hadi sasa wameshachangia zaidi ya sh. milioni 20.
Aidha, Bashungwa ametumia fursa hiyo kueleza mipango mbalimbali ya Serikali ya kupeleka miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na miradi ya maji, kufikisha umeme katika vijiji vilivyosalia, uboreshaji wa miundombinu ya Barabara na elimu.
Katika harambee hiyo, Mhe.Bashungwa amechangia Sh.milioni 10, Halmashauri imetoa Sh.milioni 20 ambapo Jumla ya michango yote iliyopatikana ni Sh.Milioni 32.1.