************************
Ni kutokana na kudaiwa kuwa chanzo cha kukwamisha usajili wa Vyama vya msingi kwa wakulima wa tumbaku
Shaka apigilia msumari wa mwisho…CCM haitokubali kuona mkulima akiendelea kuteseka
Na Mwandishi Wetu, Tabora
KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Shaka Hamdu Shaka amemuagiza Waziri wa Kilimo Hussein Bashe kumuondoa haraka Mrajisi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Tabora kwa madai amekuwa chanzo cha kukwamisha jitihada zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan za kuwainua wakulima wa zao la tumbaku na kusaabisha malalamiko kwa wakulima wa mkoa huo .
Shaka ametoa maagizo hayo leo Agosti 19,2022 wakati alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Ufumula wilayani Uyui mkoani Tabora ambapo akiwa hapo alipokea malalamiko mbalimbali ya wakulima wa zao tumbaku na miongoni mwa malalamiko ni ya kuwepo kwa urasimu wa kusajiliwa vyama vya msingi(AMCOS).
Akizungumza wakati anatoa maagizo hayo Shaka amesema amepokea malalamiko ya Mrajisi wa vyama vya ushirika mkoa wa Tabora Geophrey Chiliga kuwa na changamoto mbalimbali zinazokwamisha jitihada za wakulima. “Changamoto za bwana huyu imekuwa donda sugu , tumetoka Kaliua analalamikiiwa, tumetoka Sikonge analalamikiwa, tumetoka Urambo analalamikiwa, leo tuko Uyui watu wanalia na huyu bwana. Urasimu umekuwa mkubwa sana.
“Utitiri na ukiritimba umekuwa mkubwa sana kiasi unadumaza jitihada na huko tunakotoka hajasajili vyama kwasababu kuna mawakala wanapita chini kwa chini , Mbunge kasema na mimi taarifa ninazo wako mawakala wanapita chini kwa chini kuwaambia wakulima nenda kajiunge pale. Yeye sio kazi yake , yeye sio jukumu lake la nani akajiunge ushirika gani .
“Nani ahame wapi na aende wapi, hiyo sio kazi yake hapa kuna vyama vya ushirika 18 havijasajaliwa , amesajili saba tu na hivyo saba kwasababu ya mawakala wake na inaonekana kuna mazingira ya rushwa yanatengenezwa wakati Serikali inapiga vitaa”amesema Shaka na kuongeza ujanja ujanja huo unaonekana kuna baadhi ya watu wanajitengenezea kipato ambacho sio halali kupitia jasho la wakulima wa tumbaku.
“Maelekezo yetu kwa Wizara ya Kilimo kupitia Waziri wa Kilimo amuondoe mara moja huyu Mrajisi wa vyama vya ushirika , narudia tena maelekezo kwa Waziri wa Kilimo amuondoe, kwasababu Tabora ndio inaongoza kwa kilimo cha tumbaku hivyo hawawezi kuona jitihada za Rais Samia anatokea mtu mmoja tu anazikwamisha halafu bado akaendelea kuchekewa,”amesema Shaka.
Amesisitiza Waziri wa Kilimo watamjulisha kwamba Mrajisi huyo hafai kuwa Tabora na hivyo wampangie majukumu mengine sehemu ambayo hakulimwi kilimo cha tumbaku aende akafanye anavyotaka lakini sio Tabora. Tutalinda jasho lenu lakini tutalinda jitihada za Rais Samia anazoziweka ili kukuza zao hili la tumbaku,”alisema Shaka.
Amesema zao la tumbaku linawaheshimisha wana Tabora, limekuwa mkombozi kwao na Rais Samia ameongeza ushindani katika ununuzi kutoka kampuni mbili mpaka kampuni sita halafu, halafu anatoa mjanja mmoja anataka kukwmaisha jitihada hizo na CCM hakiwezi kukubali , hivyo watalala naye mbele.