**********************
Na Mwandishi wetu, Babati
MADEREVA wanaoendesha mabasi ya kubebea abiria wametakiwa kutoa taarifa kwa wamiliki wao pindi magari yao yanapokuwa mabovu ili yatengenezwe na siyo kuhofia kuwa watafukuzwa kazi.
Kamanda wa kikosi cha usalama barabarani Mkoa wa Manyara, Mrakibu wa polisi, SP Georgina Richard Matagi ameyasema hayo wakati akizungumza na madereva kwenye kituo cha mabasi mjini Babati.
Matagi amesema endapo dereva yeyote akitoa taarifa kwa mmiliki kuwa gari lake ni bovu na linahitajika kufanyiwa matengenezo ila akafukuzwa kazi ajulishwe ili aingilie kati.
Amesema mmiliki yeyote atakayemfukuza kazi dereva kwa sababu ya kupewa taarifa kuwa gari lake ni bovu, atamrudisha kupitia mamlaka aliyonayo pindi akipewa taarifa.
“Ninatoa namba zangu za simu ili dereva atakapokutana na ugumu huo anipe taarifa na nitalifanyia kazi na kuhakikisha nailinda kazi yake asifukuzwe ili gari litengenezwe na abiria wasafiri salama,” amesema.
Hata hivyo, amewataka madereva hao kuzingatia sheria za usalama barabarani ikiwemo kutii alama za vibao vinavyoelekeza mwendo ikiwemo kilomita 50 kwa saa na kilomita 80 kwa saa na mwendo kasi.
“Madereva msiyapite magari sehemu hatarishi, msichezee vifaa vya kudhibiti mwendo na mabasi yaendayo masafa marefu lazia liwe na madereva wawili, makondakata kuvaa sare na kuheshimu abiria na kuwa na huduma bora kwa mteja,” amesema.
Amesisitiza kutumikwa kwa tiketi za kielektroniki na kila abiria ahakikishe anakuwa nayo na amewaonyesha abiria namba za simu watakapohitaki msaada pale dereva atakapokosea na kutoa taarifa ya siri na atalindwa na huduma bora itapatikana.