************
– Amuhakikishia Rais Samia na Kamisaa wa Sensa kuwa Dar es salaam itafanya Vizuri.
– Ataka Mabalozi wa Mitaa kushirikishwa kujenga hamasa.
– Wenyeviti wa Mitaa wamuahidi hawatomuangusha.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Amos Makalla Leo amekutana na Wenyeviti wa Mitaa na Watendaji wa Kata na Mitaa kwaajili ya kuweka mipango thabiti ya kuhakikisha Zoezi la Sensa ya watu na Makazi linafanyika kwa ufanisi mkubwa na mafanikio makubwa Jijini humo.
Akizungumza na Watendaji hao, RC Makalla amewaelekeza kutumia siku chache zilizosalia kutambua mipaka ya maeneo yao ili waweze kuwaelekeza Makarani wa sensa.
Aidha RC Makalla amesisitiza wahusika wa zoezi Hilo kutumia lugha nyepesi na yenye ushawishi kwa Wananchi wa Makundi maalumu ikiwemo Watoto wa mitaani, Ombaomba na watumiaji wa dawa za kulevya ili watoe ushirikiano.
Kuhusu suala la ulinzi na usalama wakati wote wa zoezi, RC Makalla amewahakikishia kuwa Vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga vizuri kuhakikisha hakuna dosari wala uhalifu utakaojitokeza.
Pamoja na hayo RC Makalla amesema ana Imani kubwa na Watendaji wa Kata na Mitaa kwakuwa hawajawahi kumuangusha kwenye jambo lolote hivyo amemuhakikishia Rais Samia na Kamisaa wa Sensa kuwa Dar es salaam itafanya Vizuri.
Kwa upande wao Wenyeviti na Watendaji wa Kata na Mitaa wamemuhakikishia RC Makalla kuwa watahakikisha wanalibeba kwa umakini zoezi Hilo na kuhakikisha linafanikiwa.