*****************
Na Mwandishi Wetu
RAIS Samia Suluhu Hassan na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Camilius Wambura wameshauriwa kuwapandisha vyeo na mishahara askari polisi wanaofanya kazi kwa bidii na uadilifu kama njia muhimu ya kulijenga jeshi imara na la kisasa.
Ushauri huo umetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Maaskofu na Mashehe ya Maadili Amani na Haki za Binadamu kwa Jamii ya Madhehebu ya Dini nchini Askofu William Mwamalanga wakati akizungumza na viongozi wenzake wa dini jana, mkoani Mbeya.
Amesema viongozi hao wanapaswa kutumia taarifa za utendaji wa askari ambao wanaonesha kuwa na weledi, bidii, uadilifu na nidhamu wakapandishwa vyeo na mishahara ili kuwa fundisho kwa wengine.
Mwenyekiti huyo amesema katika nchi zilizoendelea zinatumia kigezo cha kuwapa mishahara mizuri wafanyakazi wanaofanya vizuri, hivyo Tanzania inapaswa kufuata misingi hiyo.
Amesema maadili na uadilifu kwa askari polisi ni muhimu ili kuhakikisha jeshi hilo linaendeshwa kwa weledi.
Askofu huyo amesema wanashauri Chuo cha Mafunzo ya Polisi Moshi (CCP), kiwe ni mahali pa kuimarisha maadili na uadilifu kwa askari polisi wanafunzi na wale ambao wanafeli somo hilo arudishwe nyumbani.
Aidha Askofu Mwamalanga, amekemea vikali tabia ya baadhi ya wananchi na wanasiasa wanaochochea chuki dhidi ya polisi na kuwataka wasaidie jeshi hilo ili kuleta ufanisi.
Mwamalanga ameishauri jamii kutoa taarifa za kweli ili kukomesha uhalifu na kuvunja mitandao ya uhalifu wa pikipiki maarufu bodaboda.
“Sisi viongozi wa dini kote nchini tukitoa ushirikiano kwa jeshi la polisia uadilifu na maad yataongezeka na askari watatokomeza uhalifu,” alisema.
Askofu Mwamalanga alitoa wito kwa viongozi wa dini kutojihusisha na uhalifu ametoboa siri pale alipowataja baadhi ya viongozi wa dini kujihusha na vitendo vya uhalifu ndiyo maana watu kama hawa hawezi kwenda polisi kuwataja wahalifu.
“Tumekubaliana kila dhehebu la dini kanisa na msikiti lazima wawe na mtandao wa vijana unaopambana na uhalifu na ili kutoa taarifa kwa jeshi la polisi pale wabapobaini vitendo vya uhalifu,” alisema.
Alisema jeshi la Mkoa wa Mbeya linafanyakazi kubwa, ila changamoto iliyopo ni uchache wa vitendekazi, hivyo wanashauri Serikali kuyawezesha jeshi hilo.