Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri – Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi akizungumza na viongozi kutoka mkoa wa Dodoma na Mkoa wa Singida wakati wa makabidhiano ya Mwenge wa Uhuru kati ya uongozi wa mkoa wa Dodoma na mkoa wa Singida yaliyofanyika wilaya ya Bahi, eneo la Sokoni Dodoma, Agosti 16, 2022. Kulia ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri – Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu Prof. Jamal Katundu.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule akikabidhiwa Mwenge wa Uhuru na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Peter Serukamba yaliyofanyika wilaya ya Bahi, eneo la Sokoni, mkoani Dodoma.
PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU
(KAZI, VIJANA, AJIRA NA WATU WENYE ULEMAVU)
***********************
Na: Mwandishi Wetu – DODOMA
Mbio za Mwenge wa Uhuru 2022 zimesaidia kwa kiasi kikubwa kufanikisha kukusanya shilingi Milioni 847.6 na kuzirejesha serikalini ikiwa ni fedha zilizotolewa na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana kwa ajili ya mikopo yenye riba nafuu kwa Vijana, Wanawake na Watu wenye Ulemavu.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi hii leo Agosti 16, 2022 wakati wa makabidhiano ya Mwenge wa Uhuru kati ya uongozi wa mkoa wa Dodoma na mkoa wa Singida yaliyofanyika wilaya ya Bahi, eneo la Sokoni Dodoma.
Mheshimiwa Katambi alieleza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan imeweka mipango Madhubuti ya kuweza kuhakikisha kila mwananchi haachi nyuma katika ujumuishwi wa uchumi, hivyo wakimbiza mwenge wa uhuru kwa mwaka 2022 wamekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha fedha hizo zinarejeshwa ili vijana wengine waweze kunufaika.
“Mbio za Mwenge wa Uhuru si jambo la mzaha, ni ujumbe wa Mheshimiwa Rais na ni jicho katika kuhakikisha maendeleo yanakuwepo. Sasa wewe fanya mchezo utakwenda na mwenge, usipotekeleza majukumu yako, kupunguza uzembe ubadhilifu, utakufuata na kukuchukulia hatua, hivyo ni vyema kila mmoja akawe makini katika eneo lake,” alisema
Aliongeza kuwa, hadi kufikia Agost 14 mwaka huu Mwenge wa Uhuru tayari umeshatembelea jumla ya Halmashauri 135 kati ya 195 zilizopangwa kutembelewa ambapo umefanikiwa kukagua na kuweka mawe ya msingi katika miradi 941 yenye thamani ya Sh bilioni 551.7, kati ya hiyo miradi 64 yenye thamani ya Sh. Bilioni 12.5 ndio iliyobainika kuwa na dosari ikiwemo kukosa nyaraka na changamoto mbalimbali za kiufundi.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Katambi amewapongeza wakimbiza mwenge wa uhuru kwa kuendelea kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi katika kushiriki Sensa ya Watu na Makazi kwa maendeleo ya taifa.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule baada ya makabidhiano ya mwenge wa alisema Mwenge huo ukiwa ndani ya mkoa wa Dodoma utakagua miradi 39 na utakimbuzwa kwa muda wa siku 8 katika mkoa wa Dodoma kwenye Halmashauri zote 7.
Akizungumza awali, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Sahil Gelaruma amewataka viongozi wa mkoa wa Dodoma kuhakikisha miradi yote itakayokaguliwa taarifa ziandaliwe vyema sambamba na kuwa na nyaraka zote muhimu ili kujiepusha na mkanganyiko wakati wa ukaguzi.
Akiongelea kuhusu fedha zikizotolewa na Serikali Kuu kupitia mfuko wa maendeleo ya Vijana na kupelekwa katika halmashauri zote nchini kwa ajili ya kutolewa mikopo yenye riba nafuu kwa vijana, katika mkoa wa Dodoma jumla ya Sh. Milioni 150 hazijarejeshwa Serikali Kuu.
“Mwenge wa Uhuru unaagiza halmashauri hizo kurejesha Fedha hizo haraka kabla mwenge wa uhuru haujapita katika halmashauri zao, mwenge wa Uhuru hautaondoka Dodoma mpaka fedha hizo zitakaporejeshwa, hivyo itakuwa ni jambo la ajabu kwa halmashauri zilizopo makao makuu ya nchi hawatafanikisha hilo,” alisisitiza kiongozi huyo.