HALMASHAURI ya Wilaya ya Ukerewe,katika kuepuka migogoro ya ardhi na wananchi imeanza kutekeleza maagizo ya serikali kwa kupima ardhi na maeneo ya taasisi za umma na kuyapatia hati miliki ili kuepusha wananchi wasiyavamie na kuanzisha shughuli za kibinadamu.
Akizungumza na leo Agosti 15,mwaka huu Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Ukerewe, Emmanuel Sherembi amesema upimaji huo wa ardhi katika maeneo ya taasisi za umma unafanyika ili kuyafanya yatambulike kisheria na kupatiwa hatimiliki.
Amesema lengo la kuendesha zoezi hilo la kupimaji wa ardhi katika maeneo ya taasisi za umma ni kuepusha migogoro ya ardhi baina ya serikali na wananchi ambao huvamia maeneo hayo na kuanzisha shughuli za kibinadamu.
Mkurugenzi huyo Mtendaji wa Wilaya ya Ukerewe amesema mradi huo ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na maagizo ya viongozi akiwemo Mh.Rais Samia Suluhu Hassan,lengo kubwa ni kuhakikisha tunaondoa migogoro ya ardhi na wananchi baadhi ambao huingilia na kuvamia maeneo ya taasisi za serikali.
“Kwa kushirikiana na Taasisi ya Mafunzo na Upimaji wa Ramani Morogoro (ARIMO),Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Mwanza na wataalamu wa Ardhi wa Halmashauri ya Ukerewe,tuna pima maeneo ya taasisi ili kuepusha migogoro baina ya serikali na wananchi wasiyavamie na kuanzisha shughuli za kibinadamu,”alisema Sherembi.
“Tunashirikiana na chuo cha Morogoro ambao tayari wametupatia wanafunzi ikiwa ni sehemu ya vitendo ya kujifunza lakini pia watafanya kazi hii ya upimaji, tutahakikisha maeneo yote ya taasisi za serikali kwa maana ya shule zote za msingi, sekondari, vituo vya afya, zahanati, maeneo yote ya vijiji na kata yote yanapimwa.
Kiongozi wa wataalamu hao,Colman Charles, amesema watapima na kusimika alama maeneo yote ya taasisi za umma zilizopo chini ya Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe,mipaka yake itafahamika kisheria na zitapewa hati,watachukua taarifa za kijiografia,watachora ramani na kuandaa majalada kwa ajili ya hati ili kuziepusha na migogoro ambapo shule,hospitali na vituo vya afya,vitachangia gharama.
“Maeneo ya taasisi za serikali wilayani Ukerewe hayakuwahi kupimwa hivyo wazo la mradi huu lilitoka Muleba wakati huo,Sherembi akiwa huko,chuo kiliwahi kumpatia vijana ili kufanikisha mpango huo na baada ya kuhamia Ukerewe akaona autekeleze hapa,”alieleza Charles.
Mpima Ardhi kutoka Ofisi ya Ardhi Mkoa wa Mwanz Paulo Ntunguru , amesema ofisi hiyo imetoa vifaa vya upimaji ardhi vya kisasa kwa ajili ya kurahisisha zoezi la upimaji wa taasisi za serikali katika halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe ili ziweze kumilikiwa kisheria na kupunguza migogoro ya ardhi ambayo inaweza ikajitokeza kwa sababu maeneo mengi ya taasisi za umma yamekuwa yakivamiwa.
Kwa upande wao Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, Joshua Manumbu pamoja na Diwani wa Kata ya Nakatunguru, Boniphace Mataba wamesema upimaji huo utasaidia kulinda ardhi za taasisi za serikali,wananchi watatambua mipaka ya taasisi hizo na hivyo kutozivamia. Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ukerewe, Joshua Manumbu pamoja na Diwani wa Nakatunguru, Boniphace Mataba walisema upimaji huo utasaidia kulinda ardhi ya maeneo ya taasisi za serikali ambapo wananchi watatambua mipaka yake na kutoyavamia.
Kwa mujibu wa Afisa Maendeleo ya Ardhi Wilaya ya Ukerewe,Paschal Malecha,mwaka huu wa fedha wamejiwekea malengo ya kupima viwanja 500 vya makazi ya wananchi ili kuepuka ujenzi holela ambapo jumla ya shule za msingi 158,sekondari 28,vituo vya afya na zahanati 38,ofisi 25 za kata na 71 za vijiji zitapimwa na kupewa hatimiliki.
“Mbali na upimaji wa maeneo ya taasisi za umma,maeneo mengine yatakayopimwa ni viwanja vya michezo vya vijiji,maeneo ya misitu,maeneo ya miradi ya serikali za vijiji,”amesema.
Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Nebuye Kata ya Ngoma Wilaya ya Ukerewe, Benedicto Malima, amemshukuru Mkurugenzi Sherembi kwa kuwapalekea timu ya wataalamu wa kupima mipaka ya shule ya Msingi Nebuye kwani baadhi ya wananchi ambao wako jirani na shule hiyo wamekuwa wakivamia na kufanya shughuli za kibinadamu.
Baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Nebuye ambako ni miongoni mwa maeneo ambayo zoezi hilo limefanyika akiwemo Felister Sulusi na John Seseja wameipongeza serikali kwa hatua hiyo yenye manufaa na itawaondolea migogoro ya ardhi baina yao na serikali.