Mkurugenzi wa Mipango,Ubora na udhibiti vihatarishi wa Mamlaka ya usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Dkt.Boniphace Nobeji,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Agosti 13,2022 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Mamlaka hiyo na mwelekeo katika mwaka wa fedha 2022/23
………………………………………….
Na Alex Sonna-DODOMA
MAMLAKA ya usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imesema kuwa ili kuweza kuhimili ushindani katika biashara ya Bandari,imeendelea kuboresha matumizi ya mifumo ya TEHAMA kuondokana na mifumo ya zamani Mifumo katika utoaji huduma za Kibandari.
Hayo yamesemwa leo Agosti 13,2022 jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Mipango,Ubora na udhibiti vihatarishi wa Mamlaka hiyo Dkt.Boniphace Nobeji,wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Mamlaka hiyo na mwelekeo katika mwaka wa fedha 2022/23 ambapo itatumia jumla ya sh.bilioni 866.051.
Dkt.Nobeji,amesema kuwa Mfumo huu kwa sasa unatumika katika shughuli za Uhasibu, Menejimenti ya Rasilimali Watu na Utawala,mfumo mwingine unaunganisha huduma za wadau wote wa huduma za kibandari nchini ambao kwa sasa wanafikia 34.
”Mfumo huu unaunganisha huduma za utekelezaji (meli na shehena) na malipo ya huduma zote kielektroniki katika Bandari za DSM, Tanga na Mtwara, unaunganisha huduma za utekelezaji na malipo ya huduma zote kielektroniki katika Bandari za Maziwa Makuu na eneo linalohudumia Meli ndogo ndogo na Majahazi-Bandari ya Dar es salaam”ameeleza
Pia ameeleza Mfumo mwingine ambao utakuwa jumuishi unaowawezesha wadau wengine kama Mawakala wa forodha kufanya malipo kwa njia za kimtandao (Mabenki, Simu na Kompyuta).
Dkt.Nobeji,amesema kuwa Mifumo yote hiyo inaimarishwa ili kuongeza ufanisi wa huduma zitolewazo na Bandari za Tanzania lakini pia kwenda sambamba na maendeleo ya Sekta ya Usafirishaji Majini Ulimwenguni.
Aidha amevitaja Vipaumbele Vitano ambavyo viko kwenye Mpango Mkakati wake wa Nne kwa mwaka 2021/22-2025/26) ambavyo ni Ujenzi wa Miundombinu ya Bandari Bora na yenye Mitambo ya Kisasa na sahihi ya Kuhudumia Meli na Shehena.
Vipaumbele vingine ni Rasilimali Endelevu (Rasilimali watu na Rasllimali Fedha),Matumizi ya Teknolojia za Kisasa kupitia Mifumo ya TEHAMA funganishi na aina za meli, shehena na pia mifumo ya kitaifa.
Amesema kuwa ni Kuongeza Shehena ya nchi jirani inayohudumiwa na bandari za Tanzania pamoja na Kuimarisha masuala ya ulinzi, usalama na mazingira katika utoaji wa huduma pamoja na kuzingatia miongozo ya kimataifa iliyoridhiwa na nchi.
Dkt.Nobeji,amesema Katika kipindi kilichoanzia mwezi Julai 2021 hadi Juni, 2022, hali ya utendaji wa Mamlaka ya usimamizi wa bandari TPA ilikuwa na Jumla ya Shehena iliyohudumiwa Katika kipindi cha Julai 2021 hadi Juni 2022, shehena iliyohudumiwa ni Tani milioni 20.665 sawa na ongezeko la asilimia 16 ya Tani milioni 17.775 milioni zilizohudumiwa mwaka uliopita (Julai 2020 hadi Juni 2021).
”Shehena ya Makasha (Twenty Foot Equivalent Unit – TEUs) Idadi ya Makasha yaliyohudumiwa kipindi cha Julai 2021 hadi Juni 2022 ilifikia Makasha (TEUs) 823,404 sawa na ongezeko la asilimia 12 ya makasha (TEUs) 735,442 yaliyohudumiwa katika kipindi kama hiki mwaka uliopita (Julai 2020 hadi Juni 2021).”amesema Dkt.Nobeji
Amesema Shehena ya Magari iliyohudumiwa katika Bandari ya Dar es Salaam kwa kipindi cha Julai 2021 hadi Juni 2022 ni 203,932 sawa na ongezeko la asilimia 38 ya magari 147,566 yaliyohudumiwa mwaka uliopita (Julai 2020 hadi Juni 2021).
“Shehena ya Masoko ya Nchi Jirani Shehena ya nchi jirani iiliyohudumiwa katika Bandari ya DSM katika kipindi cha Julai 2021 hadi Juni 2022 ni Tani 7.801 milioni sawa na ongezeko la asilimia 39.9 ya Tani 5,580 milioni iliyohudumiwa mwaka (Julai 2020 hadi Juni 2021). Nchi jirani zinazohudumiwa na Bandari ya Dar es salaam ni DR-Congo, Zambia, Malawi, Rwanda, Burundi, Uganda, Zimbabwe, Comoro na Sudan Kusini.
Katika hatua nyingine amesema kuwa Katika kipindi cha kuanzia Julai 2021 hadi Juni 2022 TPA ilifanikiwa kukusanya Jumla TZS 1.095 Trilioni sawa na asilimia 97.5 sawa na ongezeko la asilimia 20.3 ya mapato ya TZS 910.4 Bilioni yaliyokusanywa kipindi kama hiki mwaka uliopita (Julai 2020 hadi Juni 2021).
Amesema Kutokana na Juhudi za Kuboresha Mazingira ya Ufanyaji Biashara na Kuvutia wa Wekezaji Nchini, zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita Chini ya Uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
”Sekta ya Bandari imepata mafanikio makubwa Baadhi ya Mafanikio hayo kama ni Bandari ya Dar es Salaam ilipokea na kuhudumia Meli kubwa ya MV. GLAND DUKE PANAMA iliyoshusha Magari yapatayo 4,041 ikiwa ni idadi ya juu ya Magari kuwahi kuhudumiwa katika Bandari za Tanzania”amesema
Bandari ya Dar es Salaam ilipokea na kuhudumia meli ya Shaba MV PAPA JOHN ambayo ilipakia Tani Elfu Arobaini na Moja (41,000).
Amesema Bandari ya Tanga imeweza kuhudumia meli kubwa za mafuta kama ifuatavyo, MT.UACC Sila iliyoshusha tani 39,811.762, Mv.NOD JOY iliyoshusha tani 36,448 na MV.SILVER ZOE iliyoshusha tani 38,446 sawa na jumla ya tani Tani 114,707 kwa meli zote tatu hivyo kuvunja record ya Tani za mafuta zilizowahi kuhudumiwa Bandari ya Tanga. Pia, Bandari ya Tanga imehudumia meli ya clinker ya Mv.Star Fighter iliyo beba tani 49,500 ikiwa shehena kubwa kwenda Rwanda kuwahi kuhudumiwa katika Bandari ya Tanga.