Na Mwandishi Wetu, Iringa
UMATI mkubwa wa wananchi wanajitokeza kwenye ziara inayoendelea ya Rais Samia Suluhu Hassan mikoani, huku wananchi wengi wakieleza kuguswa na uwekezaji mkubwa wa serikali yake kwenye miradi ya maendeleo na ya jamii, ikiwemo sekta za afya, maji na elimu.
Rais Samia, ambaye yuko ziarani mikoa ya Mbeya, Njombe na Iringa ameacha gumzo kubwa kwenye mikoa ya nyanda ya juu Kusini.
Katika ziara yake hiyo, msafara wake umepokewa na umati mkubwa wa wananchi barabarani ambao wamejitokeza kumuona Rais, huku wengine wakitaka asimame japo awasalimie.
Wazee, wanaume, wanawake, vijana na hata watoto wamekuwa wakiacha shughuli zao kila sehemu Rais Samia anapopita na kumsubiria barabarani pamoja na kuhudhuria mikutano yake ya hadhara.
Uamuzi wa Rais Samia kutoa kipaumbele kwa wananchi wasikilizwe shida zao na kuongozana kwenye ziara yake na mawaziri kadhaa ili wajibu hoja za wananchi umepokelewa kwa furaha na wananchi.
“Kwa kweli Rais Samia tunampenda sana kwa kuwa anatujali sisi wananchi wa chini kwa kutuletea miradi mikubwa ya afya, maji na elimu,” alisema Rose Kalinga, mfanyabiashara ndogondogo wa mkoa wa Iringa.
“Tofauti na wanasiasa wengine ambao wamekuwa na desturi ya kusomba watu kwenye Fuso waende kwenye mikutano yao au kuwalipa waimbaji wa Bongo Fleva wajaze uwanja, Rais Samia amekuwa hatumii mbinu hizo wananchi wanaenda wenyewe kwa wingi kumsikiliza”,alisema.
Wabunge kadhaa wa mikoa ya Mbeya, Njombe na Iringa wamesema kuwa Rais Samia ameweka historia kwa kupeleka pesa nyingi za maendeleo mikoani kuliko wakati wowote ule kwenye historia ya nchi.