Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikata utepe wakati alipomuwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika Uzinduzi wa jengo la ofisi ya Makao Makuu ya Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) jijini Dodoma, Agosti 12, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipomuwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika Uzinduzi wa jengo la ofisi ya Makao Makuu ya Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) jijini Dodoma, Agosti 12, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Baadhi ya washiriki wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipozungumza akimuwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika Uzinduzi wa jengo la ofisi ya Makao Makuu ya Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) jijini Dodoma, Agosti 12, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
***********************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kushirikiana na madhehebu yote ya dini katika nyanja mbalimbali ili kukuza na kuimarisha ustawi wa wananchi kiuchumi na kijamii.
“Sote tumeshuhudia jinsi Serikali inavyoweka mazingira mazuri ya kuwekeza kwa ujenzi wa miundombinu muhimu ya barabara na madaraja, reli ya kisasa, vivuko, meli na usafiri wa anga. Jitihada hizi zote pamoja na kuimarisha uzalishaji wa umeme, gesi na maji hapa nchini zinafanyika kwa lengo la kuboresha ustawi wa maisha ya Tanzania.”
Mheshimiwa Majaliwa ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Agosti 12, 2022) alipomuwakilisha Mheshimiwa Rais Samia katika ufunguzi wa Jengo la Makao Makuu ya Kanisa la Tanzania Assemblies Of God (TAG) katika Chuo cha Biblia Miyuji, Dodoma. Jengo hilo litakuwa na ofisi mbalimbali za kiutendaji za TAG pamoja na kutoa mafunzo ya uzamili na uzamivu kwa viongozi na wachungaji mbalimbali kutoka Bara la Afrika na maeneo mengine duniani.
“Serikali inaelewa kwamba Maendeleo ya nchi yanahitaji ushiriki wetu sote. Tukiimarisha ushirikiano na kila mtu, tutaleta maendeleo ya Taifa. Kwa kuzingatia hayo, Serikali imekuwa ikishirikiana na Sekta binafsi zikiwemo Taasisi za dini katika kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi na kuleta maendeleo ya Taifa.”
Amesema kanisa la TAG, pamoja na taasisi nyingine za kidini zimekuwa mstari wa mbele katika utoaji wa huduma mbalimbali zinazogusa jamii kama elimu, afya na huduma nyingine muhimu kwa jamii ambazo Serikali pekee isingeweza kuzifikisha kwa wananchi mara moja.
“Kipekee nilipongeze sana kanisa la TAG kwa kutoa huduma ya elimu kupitia shule zenu za msingi na sekondari ambazo ziko ndani ya mikoa mbalimbali hapa nchini. Nimeelezwa mnazo shule za msingi 10 na shule tano za sekondari zilizokamilika na kwamba nyingine nane ziko katika hatua mbalimbali za ujenzi. Halikadhalika mnavyo vyuo vya ufundi stadi 2 lakini hamkuishia hapo sasa manataka kujenga chuo kikuu hapa Dodoma, hongereni sana.”
Akizungumzia kuhusu malalamiko ya TAG ya kucheleweshwa kumilikishwa ardhi katika eneo la Chigongwe, amemtaka Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Joseph Mafuru ahakikishe suala hilo linashughulikiwa haraka na ndani ya siku saba awasilishe taarifa kwake. TAG linataka kujenga chuo kikuu katika eneo hilo.
Naye, Askofu Mkuu wa TAG, Baba Askofu Mkuu Dkt. Barnabas Mtokambali amesema Kanisa la TAG pamoja na jukumu la kiroho la kanisa la kuwafanya watu wote waache maasi na kurejea kwa Muumba wao, pia lina wajibu wa kujihusisha na maendeleo ya kijamii yanayogusa mtu kiroho, kimwili, kiakili, kihisia, na kijamil.
“Kwa kuzingatia hayo, kanisa la TAG; katika mpango mkakati wake wa miaka 13 (2020 – 2033), limeweka mkakati wa kujenga shule za msingi na sekondari kila mkoa, vituo vya watoto yatima, vituo vya afya kila mkoa, visima wya maji vijijini, vyuo vya elimu na afya, chuo kikuu hapa Dodoma na miradi mingine ya maendeleo ya kanisa na jamii kwa ujumla.”
Kadhalika, Askofu Dkt. Mkotokambali ametumia fursa hiyo kumpongeza Mheshimiwa Rais Samia kwa kudumisha amani na mshikamano wa kitaifa, pamoja na kusimamia jitihada mbalimbali za kuhakikisha miradi yote ya kimkakati inasonga mbele na kuibua miradi mingine mipya.