Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba akiangalia Skimu hiyo wakati wa ukaguzi.
Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda ambaye ana kaimu nafasi ya ukuu wa wilaya ya Manyoni akizungumza katika mkutano wa hadhara Kijiji cha Itagata.
Na Dotto Mwaibale, Itigi.
SERIKALI mkoani Singida imesema itawanyang’anya na kuyagawa kwa wengine
wakulima waliopewa mashamba katika Skimu ya Umwagiliaji Itagata iliyopo katika
Halmashauri ya Wilaya ya Itigi ambapo wametelekeza ekari 169 bila kuzilima.
Msimamo huo ulitangazwa jana na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba
baadaya kuitembelea skimu hiyo ambayo serikali ilitumia zaidi ya Sh.bilioni 2.1
kuijenga lakini idadi kubwa ya wakulima hawalimi huku wengine wakiyakodisha
mashamba kwa watu wengine.
Alisema serikali haiwezi kukubali kuona katika mradi huu ambao serikali
ilimewekeza mabilioni ya fedha ekari 40 tu ndizo zonazolimwa kati 209
walizogawiwa wakulima ambao ni wananchama wa umoja wa umwagiliaji Itigi.
“Serikali imewekeza fedha nyingi sana kwenye mradi huu lakini hatujautendea
haki na hata maji yanafika hapa lakini hapalimwi, hii haikubaliki lazima watu walime
ili kuisaidia Serikali kupata mapato na Tume ya Umwagiliaji nao wapate tozo
zao,” alisema.
Alisema matumaini ya serikali ni kuona eneo lote linalimwa wakati wa
kiangazi na masika ili baada ya hapo ijengwe hoja ya kutaka kuongezewa eneo
jingine la kulima.
Kufuatia hali hiyo,Mkuu wa Mkoa alimwagiza Mwenyekiti wa Halmashauri ya
Itigi, Diwani na Mtendaji Kata kuandaa mkutano ili waweze kuwajua watu wasio na uwezo
wa kulima wasikodishe mashamba wapewe wengine wenye uwezo wa kulima.
“Mwezi wa tisa mwenyekiti andaa mkutano na wanachama wako ili tuje
tujue nani analima na nani halimi ili wale ambao hawalimi tuwaondolee mashamba
tuwape wengine ambao watalima na kuipa Serikali mapato pamoja na Tume ya
umwagiliaji,” alisema.
Serukamba alisema wakulima lazima watambue kuwa faida atakayoipata mkulima
kupitia kilimo kwenye skimu hiyo itamrahishia maisha kiuchumi ataweza kuhudumia
familia, kulipa bima ya afya pamoja na
kuchangia maendeleo ya taifa lake.
“Kuna watu kule Dodoma hawana maji na wangetamani kulima lakini nyie
mumepata maji lakini hamtaki kulima hatueleweki unayetaka kulima
vitunguu,mahindi mpunga lima,” alisema.
Serukamba alisema serikali imetoa mbolea ya ruzuku ambayo sasa itakuwa imauzwa
Sh.70,000 hivyo wakulima wajifunze na matumizi ya mbolea katika kilimo hicho.
Mkulima katika skimu hiyo, Chacha
Marwa alisema changamoto inayokabili
wakulima wengi kutolima ni kushindwa kutambua aina ya udongo pamoja na baadhi ya Wanachama wa umoja huo wa umwagiliaji waliopewa
mashamba kuyakodisha kwa watu wengine.
“Mhe. Mkuu wa Mkoa sisi huu udongo unatuchanganya sana tunashindwa
kuelewa tulime mbegu gani tunaomba mtusaidie kutupimia udongo wetu,”
alisema.
Chacha alisema kuwa baadhi ya
wasimamizi wa skimu hiyo sio waaminifu kwa wanachama wao jambo linalopelekea
washindwe kufanya shughuli za kilimo cha umwagiliaji kwani wamekuwa wakikodisha
mashamba na kuwanyima fursa wengine.
Awali Mwenyekiti wa Umoja wa Umwagiliaji Itagata, Stephano Mbonde alisema
kuwa mashamba yenye ukubwa wa Ekari 209 yaligawiwa kwa wanachama 321 ambapo
ekari 106 ziligawiwa kipindi cha masika.