Baadhi ya mabanda yanayotumika kwa ajili ya maonyesho ya wakulima nanenane kata ya Msamala manispaa ya Songea.
Muonekano wa sehemu ya nane nane kata ya msamala ambayo serikali kupitia Manispaa ya Songea inataka kutumia eneo hilo kama mji wa kiserikali ambapo kutajengwa ofisi za idara na taasisi mbalimbali za serikali.
Bustani za mboga katika eneo la nane nane Manispaa ya Songea eneo ambalo kuanzia mwaka ujao halitatumika tena kwa shughuli za maonesho ya wakulima ili kupisha ujenzi wa ofisi za taasisi na idara mbalimbali za serikali.
Baadhi ya vijana kutoka maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma wakiangalia njiwa katika moja ya banda katika maonyesho ya wakulima nane nane ambayo kimkoa yalifanyika katika viwanja vya nane nane Manispaa ya Songea.
Mabanda ya maonyesho ya wakulima katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma kama yanavyoonekana.
…………………………
Na Muhidin Amri,Songea
MANISPAA ya Songea mkoani Ruvuma,imepanga kubadilisha eneo la viwanja vya maonesho ya wakulima nane nane kata ya Msamala kuwa sehemu ya mji wa kiserikali.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Andambike Kyomo, wakati akizungumza na waandishi wa Habari wakati wa maonesho ya wakulima ambayo kimkoa yalifanyika Manispaa ya Songea.
Alisema kutokana na mji wa Songea kukua kwa kasi kubwa na mahitaji ya huduma za kijamii kuwa makubwa,serikali imepanga kubadilisha matumizi ya eneo hilo na kuwa mji wa kiserikali,na kuanzia mwaka ujao maonesho ya wakulima yatafanyika kata ya Mwengemshindo.
Kwa mujibu wa Kyomo ambaye ni mkuu wa idara ya uchumi na mipango ni kwamba, katika eneo hilo hakutaruhusiwa majengo ya chini, bali taasisi zote zinatakiwa kuwa na majengo ya ghorofa moja na kuendelea.
Alisema,mpaka sasa wamepokea maombi kutoka taasisi mbalimbali ikiwamo Mahakama kuu kanda ya Songea,wakala wa maji (Ruwasa)ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Songea na Magereza Mkoa wa ruvuma Songea ambazo zimetuma maombi ajili ya kujenga ofisi zake katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa Kyomo,kuleta ofisi za serikali katika eneo hilo kutaleta manufaa makubwa kwa jamii inayozunguka katika eneo hilo na kata jirani ya Mshangano, ambapo thamani ya ardhi itaongezeka,uwekezaji wa nyumba za kuishi,biashara na miundombinu itaongezeka kwa kasi kubwa.
Aidha alisema,katika bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 Manispaa ya Songea imeshatenga Sh.milioni 500 za kuanzia kwa ajili ya kujenga ofisi zake ambazo zitakuwa ghorofa mbili na mpango uliopo ni kuhama katika ofisi za sasa ambazo zimejengwa tangu mwaka 1976.
“mahitaji ya mwaka 1976 hayatakuwa sawa na mahitaji ambayo tunayo mwaka 2022,sasa tunahitaji kuwa na ofisi nyingi ili ziweze kutosheleza utoaji wa huduma kwenye taasisi zetu za Halmashauri”alisema.
Kyomo alisema, baada ya kumaliza ujenzi wa ofisi ya Halmashauri wanatarajia ofisi ya wakuu wa idara na vitengo kuwa eneo moja hivyo mwananchi akifika kupata huduma atapata kwa urahisi na haraka zaidi tofauti na sasa ambapo baadhi ya ofisi zimetawanyika”alisema Kyomo.
Baadhi ya wananchi wa Manispaa ya Songea,wameipongeza Manispaa ya Songea kutokana na kuonesha nia ya kubadili matumizi ya eneo hilo.
Abdul Ngonyani alisema,eneo la nane nane Msamala ni kati ya maeneo machache muhimu katika manispaa ya Songea,lakini kwa muda mrefu limeshindwa kutumika vizuri kutokana na changamoto mbalimbali ikiwamo ya kuzungukwa na makazi ya watu.
Ngonyani alisema,kama serikali itafanikiwa kutimiza adhima yake kwa kuhamishia shughuli za maonyesho ya wakulima kata ya Mwengemshindo na eneo la Msamala kujengwa ofisi za serikali itasaidia kutanua mji wa Songea na kuboresha shughuli hizo za maonyesho ya wakulima.
Grace Ngongi mjasirimali kutoka wilaya ya Mbinga,ameiomba Serikali ya mkoa wa Ruvuma kuboresha maonyesho ya wakulima ili yaendane na ukubwa wa mkoa huo badala ya kuwekeza nguvu kubwa maeneo ya kanda kwa kuwa siyo wakulima wote wanaweza kwenda na kujifunza mbinu za kilimo bora.
Aidha,ameipongeza taasisi ya utafiti wa kilimo(TARI)kituo cha Naliendele mkoani Mtwara kwa kushiriki maonyesho yam waka huu kwani wakulima wengi wamepata faida na kujifunza kilimo cha mazao mbalimbali kama vile muhogo,korosho na mazao mengine ya chakula na biashara.