Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis akitoa maelekezo wakati alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua shughuli za uchenjuaji kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu katika Kijiji cha Nayu wilayani Chamwino mkoani Dodoma leo Agosti 10, 2022.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis akikagua sehemu ya kuchenjulia dhahabu wakati alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua shughuli za uchenjuaji kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu katika Kijiji cha Nayu wilayani Chamwino mkoani Dodoma leo Agosti 10, 2022.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis (kushoto) akiwa katika ziara ya kukagua sehemu ya kuchenjulia dhahabu wakati alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua shughuli za uchenjuaji kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu katika Kijiji cha Nayu wilayani Chamwino mkoani Dodoma leo Agosti 10, 2022.
************************
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis ametoa mwezi mmoja kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu katika Kijiji cha Nayu wilayani Chamwino mkoani Dodoma kufuata vibali vya kulinda mazingira.
Ametoa agizo hilo leo Agosti 10, 2022 wakati alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua mazingira katika eneo hilo kutokana na wachimbaji hao kudaiwa kufanya shughuli hizo bila taratibu na kuhatarisha usalama wa mazingira na afya.
Alisema imebainika kuwa kuna shughuli za uchimbaji na uchenjuaji zinafanyika bila kufuata taratibu zikiwemo za utiririshaji ovyo wa maji yasiyo salama na kuelekea kwenye vyanzo vya maji hivyo kuhatarisha afya za wananchi.
Mhe. Khamis alisema kuwa Serikali inatambua shughuli halali za kujipatia kipato zinazofanywa na vijana hususan katika shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa dhahabu lakini ni lazima ziendane na sheria za utunzaji wa mazingira.
Amewaelekeza wachimbaji hao wadogo kufuatilia vibali katika Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Mamlaka ya Bonde la Wami-Ruvu ili kupata vibali vya kufanya shughuli hizo.
“Kuna mto unapita hapa lakini tunaona kuna shughuli za kibinadamu zikiwemo uchenjuaji zinafanyika hapa sasa kemikali za sumu zinatoka hapa na kusambaa katika maji ya mto hali inayoweza kuhatarisha afya za wananchi,” alisema Mhe. Khamis.
Pia, naibu waziri aliwataka wananchi kutunza vyanzo vya maji na kuepuka kufanya shughuli za kibinadamu zikiwemo ufugaji na kilimo kwani ndio chanzo kikubwa cha uchafuzi wa maji na mazingra kwa ujumla.
Sambamba na hilo alihamasisha zoezi la upandaji na utunzaji wa miti katika maeneo yao kwani ndio chanzo cha kunyesha kwa mvua na hivyo kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wake Meneja wa Kanda ya Kati wa NEMC Dkt. Franklin Rwezamila alisema wachimbaji wadogo wa dhahabu wanaojihusisha na shughuli za uchenjuaji wana wajibu wa kufuata taratibu za kimazingira.
Alisema afya ya binadamu ni muhimu kulindwa na pia mazingira yanayozunguka yanapaswa pia kulindwa hivyo ni muhimu kutekeleza maelekezo ya wataalamu wa mazingira.
“Wananchi wanategemea maji kutoka kwenye vyanzo mbalimbali ili waweze kuyatumia kwa mahitaji yao lakini wawekezaji nao wanapaswa kufuata taratibu za kimazingira,” alisema.
Naye Meneja Msaidizi Rasilimali za Misitu Kanda ya Kati Bi. Patricia Manonga alisema pamoja na kuwa wachimbaji hao kuwa na leseni za uchimbaji lakini wanapaswa kupata kibali cha matumizi ya eneo hilo.