Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga Bw. Donasian Kessy akitoa taarifa ya utekelezaji wa kazi zilizotekelezwa na TAKUKURU kwa kipindi cha robo ya nne ya Mwaka wa fedha 2021/2022.
Na Stela Paul – Shinyanga
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga imewataka wananchi kutofumbia macho vitendo vya rushwa kwa kutoa taarifa kama wataona kuna vitendo vyovyote vinavyoashiria ubadhilifu wa miradi ya maendeleo.
Rai hiyo imetolewa leo Jumatano Agosti 10,2022 na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga Bw. Donasian Kessy wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa kazi zilizotekelezwa na TAKUKURU kwa kipindi cha robo ya nne ya Mwaka wa fedha 2021/2022.
Amesema wananchi wanatakiwa kutoa ushirikiano kwa serikali ili kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa inakamilika kwa ubora huku akibainisha kuwa wamejipanga kukamilisha majukumu yao kwa kujielekeza zaidi kwenye ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha inatekelezwa kwa thamani halisi ya fedha inayotolewa.
“TAKUKURU inaendelea kutoa wito kwa wananchi wote wa Mkoa wa Shinyanga kutoa ushirikiano kwa serikali yao, kuhakikisha miradi yote inayoendelea katika Mkoa wetu inakamilika kwa ubora, kama wataona kuna vitendo vyovyote ambavyo vinaashiria ubadhilifu wa miradi hiyo watoe taarifa”, Kessy amesema.
Amesema katika kipindi cha Aprili – Juni,2022 Dawati la Uchunguzi lilipokea taarifa 29 za malalamiko lakini taarifa 23 zilihusu rushwa kutoka sekta mbalimbali ambapo mpaka sasa taarifa tano zimekamilisha uchunguzi.
“Kwa upande wa Dawati la Uchunguzi, tumepokea taarifa 29 za malalamiko, ambapo taarifa zinazohusu rushwa zilikuwa 23 na zisizohusu rushwa zilikuwa 6.Taarifa zinazohusu rushwa zilihusisha sekta zifuatazo: serikali za mitaa (8), ujenzi (6), polisi (3), maji (2), elimu (2) na biashara (1)”, amesema Kessy.
“Kesi zinazoendelea mahakamani ni 7 kati ya hizo kesi mpya ni 3 na katika kipindi hicho cha Aprili – Juni, kesi 10 ziliamuliwa mahakamani na kesi 7 zilishinda kwa watuhumiwa kutiwa hatiani na kati ya kesi hizo mtuhumiwa mmoja alihukumiwa kwenda jela miaka mitatu.