Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Zainab Chaula akizungumza na Wazee wanahudumiwa katika Makazi ya Wazee Njoro Moshi mkoani Kilimanjaro wakati wa ziara yake kukagua huduma zinazotolewa katika Makazi hayo.
Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Zainab Chaula akisalimiana na mmoja wa Mzee anayehudumiwa katika Makazi ya Wazee Njoro Moshi Mkoani Kilimanjaro wakati wa ziara yake kukagua huduma zinazotolewa katika Makazi hayo.
Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WMJJWM
****************************
Na WMJJWM Moshi
Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Zainab Chaula, amewataka Maafisa Maendeleo ya Jamii ngazi za Mikoa na Halmashauri kuhamaisha vikundi vya maendeleo katika maeneo yao ili Shabaha yakuwakwamua wananchi kiuchumi iweze kutimia.
Dkt. Chaula ameyasema hayo wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro alipotembelea Makazi ya Wazee Njoro na kuhimiza Maafisa hao kuhamasisha vikundi vya maendeleo ili viweze kutafuta fursa mbalimbali za mikopo na masoko zitakazosaidia kuwakwamua kiuchumi.
Ameongeza kuwa Serikali inaendelea na jitihada za kutafuta masoko ya nje kwa bidhaa mbalimbali ikiwemo mbogamboga na matunda hivyo akawataka Maafisa hao kuwahimiza vijana kujiunga katika vikundi vya maendeleo ili kutumia fursa hizo kwa maendeelo ya jamii na taifa kwa ujumla.
“Tukiisaidia jamii ikaendelea na kuwa na miradi ya maendeleo ya mtu binafsi na vikundi itawezesha Jamii kujikwamua kiuchumi na kuwa na kipato zaidi itakayosaidia kutunza familia hasa Wazee ” alisema Dkt Chaula
Kaimu Afisa Mfawidhi wa Makazi hayo Christa Katorogo, alisema lengo la Mkazi hayo ni kutoa huduma muhimu kwa wazee wasiojiweza na wasio na ndugu kwa kuwapa faraja na amani katika maisha yao na Makazi hayo yanahudumia wazee 16 waopatiwa huduma za chakula na afya.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri wa Wazee Taifa Mzee Lameck Sendo amewaasa vijana kuchangamkia fursa za maendeleo katika maeneo yao kwa kujituma na kujiwekea akiba na kujindaa na uzee kwani uzee na kuzeeka haukwepeki na hivyo wajiandalie maisha baada ya kustaafu.