***************************
Na Mwandishi wetu, Mirerani
WACHEZAJI wa kituo cha vijana cha Tanzanite Sports Academy cha Mirerani wilayani Simanjiro ambacho kimekwenda jijini Dodoma kushiriki michuano ya vijana ya Kashasha Youth tournament ambayo yameanza leo Alhamisi huku yakipangwa kufikia tamati Jumapili hii, wamejinasibu kuwa watarejea na ushindi.
Mkurugenzi wa Tanzanite Sports Academy, Charles Mnyalu amesema mashindano hayo yameandaliwa na Fountain Gate Academy ya jijini Dodoma ambapo yanatimua vumbi kwenye uwanja wao wa Fountain Gate Arena.
Ameongeza kuwa wamejindaa vyema kufanya kweli na kutwaa ubingwa kwani kutokana na namna vijana hao walivyo hawaoni timu ya kuweza kuwazuia licha ya kwamba lengo ni kuibua vipaji.
Amesema mashindano hayo ni mazuri kwani ni daraja la kuvusha wachezaji wadogo kisoka kupata fursa ya kuonyesha vipaji na kuweza kuonekana kwa mawakala na vilabu mbalimbali ambayo inapelekea na wao kutimiza ndoto zao.
Mnyalu ameweka wazi kuwa wameamua msimu huu timu zao mbili za vijana walio chini ya umri wa miaka 13 na 20 kushiriki katika michuano hiyo ili kuweza kuonyesha vipaji vyao lakini pia kuwakutanisha na wachezaji wengi kutoka vituo tofauti kwani sera yao ni kutoa nafasi kwa vijana kuonyesha vipaji vyao kwa ajili ya faida ya baadaye kwa Manyara.
“Kwa muda mfupi ambayo kituo chetu imeanzishwa mafanikio makubwa yameonekana kupitia katika mashindano kama haya ya vijana kwani tumeweza kumtoa mlinda lango wa U-17 ambaye hivi sasa yuko nchini Uturuki kwa majaribio kwenye moja ya timu inayoshiriki ligi daraja la kwanza,” amesema Mnyalu.
Kwa upande wake Mengi Laizer ambaye ni mtoto wa Bilionea wa madini ya Tanzanite Saniniu Laizer amesema wapo katika mipango ya kurudisha morali ya soka mkoani Manyara ambayo kwa sasa imepotea.
Mengi akimwakilisha bilionea huyo katika halfa ya kuwaanga wachezaji wa kituo cha vijana cha Tanzanite Soccer Academy cha Mirerani wilayani Simanjiro ambacho kimekwenda jijini Dodoma kushiriki michuano ya vijana ya Kashasha Youth tournament.
Mengi amesema mikakati waliyonayo kwa sasa ni kuwaunga mkono wadau wote ambao wameonyesha nia ya kufufua tena soka la Simanjiro ambayo lipo chini.
Ameongeza kuwa kama wadau mchango wao ni kuhakikisha wanawashika vijana mikono ili watimize ndoto zao huku akiunga mkono safari kwa kutoa Sh500,000 na kuwataka kurudi na ushindi ambapo pia amewahidi kuendelea kuwawezesha kupitia vifaa vya michezo.
Diwani wa kata ya Naisinyai, Taiko Kurian Laizer amesema kama serikali kwa kushirikiana na wadau hasa ambao wamegeukia soka la vijana anaamini morali na hamasa ambayo imeshuka kwa sasa itarejea na kuwa kama zamani ambapo walikuwa ni wilaya tishio kisoka Manyara.
“Hata kwenye vikao vyetu vya baraza la madiwani nitaipeleka hii lakini pia mimi mwenyewe nitajitahidi kushirikiana na wadau wa michezo ili wilaya yetu irejeshe tena makali yake” amesema Taiko.
Katibu mwenezi wa CCM Kata ya Naisinyai Simon Kinyasi amewaasa wachezaji hao kutanguliza nidhamu kwani hakuna mafanikio yoyote bila kuwa na nidhamu.