Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini akisalimiana na Maafisa wa Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es Salaam (DPA), wakati alipokuwa anawasili kuzungumza na viongozi pamoja na kukagua miradi ya maendeleo katika chuo hicho kilichopo Kurasini, jijini Dar es Salaam, leo. Katikati ni Mkuu wa Chuo, SACP Lazaro Mambosasa. Ameviagiza Vyuo vya Polisi nchini kuupitia mtaala wa mafunzo ili kujua kwa kiwango gani unajaribu kugusa changamoto mbalimbali zinazoonekana katika utekelezaji wa kazi za Maafisa na Askari katika jamii.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini akizungumza na Viongozi wa Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es Salaam (DPA), kabla ya kuanza kukagua miradi ya maendeleo katika chou hicho, Kurasini, jijini Dar es Salaam, leo. Wapili kulia ni Mkuu wa Chuo hicho, SACP Lazaro Mambosasa. Ameviagiza Vyuo vya Polisi nchini kuupitia mtaala wa mafunzo ili kujua kwa kiwango gani unajaribu kugusa changamoto mbalimbali zinazoonekana katika utekelezaji wa kazi za Maafisa na Askari katika jamii.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini (kushoto) akionyeshwa na Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es Salaam (DPA), SACP Lazaro Mambosasa, moja ya bweni kati ya manne yanayojengwa, wakati alipofanya ziara ya kukagua miradi ya maendeleo katika Chuo hicho, Kurasini, jijini Dar es Salaam,
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini (wapili kushoto) akiangalia mbwa akiwa ndani ya banda katika Kikosi cha Mbwa na Farasi wakati alipofanya ziara Makao Makuu ya Kikosi hicho, Kurasini, jijini Dar es Salaam, leo. Kushoto ni Kamanda wa Kikosi hicho, SP Majura Kyariga.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini akizungumza na Maafisa na Askari wa Kikosi cha Mbwa na Farasi wakati wa ziara yake Makao Makuu ya Kikosi hicho, Kurasini jijini Dar es Salaam, leo. Kushoto ni Kamanda wa Kikosi hicho, SP Majura Kyariga.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini akimpongeza Kamanda wa Kikosi cha Mbwa na Farasi, SP Majura Kyariga, baada ya kumaliza kusoma taarifa yake, wakati alipofanya ziara Makao Makuu ya Kikosi hicho, Kurasini jijini Dar es Salaam, leo. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
………………………………
Na Mwandishi Wetu, MoHA
NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini ameviagiza Vyuo vya Polisi nchini kuupitia mtaala wa mafunzo ili kujua kwa kiwango gani unajaribu kugusa changamoto mbalimbali zinazoonekana katika utekelezaji wa kazi za Maafisa na Askari katika jamii.
Akizungumza baada ya kumaliza ziara yake ya kukagua miradi ya Jeshi la Polisi katika Chuo cha Taaluma ya Polisi na Kikosi cha Mbwa na Farasi, Kurasini jijini Dar es Salaam, leo, Sagini alisema kuna baadhi ya tabia zinazoonyeshwa na baadhi ya askari zinauzunisha sana na kujiuliza kama kweli wamepata mafunzo.
“Nimewapa changamoto, wao ndio Chuo cha Maafisa na Viongozi wa Jeshi letu la Polisi, nimewataka waangalie mtaala wao kwa kiwango gani unajaribu kugusa changamoto tunazoziona katika utekelezaji kazi wa maafisa na vijana wetu askari Polisi, kwasababu hawa ndio viongozi, wauongezee ‘pakeji’ ya weledi itakayoweza kutusaidia vijana wanaohitimu, wawasaidie wale askari wanaotoka kwenye kozi zile za msingi watekeleze majukumu yao kwa mujibu wa PGO (Kanuni za Jeshi la Polisi) na maadili mema,” alisema Sagini.
Naibu Waziri Sagini aliongeza kuwa, wamekubaliana na viongozi wa chuo hicho kuwa, lazima kuwepo na mkakati wa kuimarisha mafunzo na pia wawe na mfumo wa ufuatiliaji wa kuona kwamba mafunzo wanayotoa kwa wale waliopewa mafunzo kweli wanatekeleza wajibu wao.
“Kama inavyosema ‘theory’ (nadharia) za majeshi kwamba ‘We don’t have a bad soldier but we have a bad general’ kwamba wale viongozi wetu wa hizi Taasisi wanapaswa kuonyesha ‘leadership’ (uongozi) ili wadogo zao waweze kujifunza mwenendo mwema wa utekelezaji wa majukumu.
Aidha, Sagini ameridhishwa na kazi ya ujenzi wa mabweni manne katika Chuo hicho ambayo yapo hatua ya mwisho kukamilika japo kuna ucheleweshaji wa miezi mitatu hadi mitano lakini kutokana na fedha zilitoka mwishoni mwa mwaka hazikuweza kutumika mpaka mifumo ilipofunguliwa mwezi Julai.
“Kwasababu fedha wanazo, nasisi tunatamani kuona fedha zote zinazotolewa na Serikali yar ais Samia Suluhu Hassan inafanyakazi iliyokusudiwa kwa wakati, wafanyekazi bila kuchoka usiku na mchana, wakamilishe ili yae mabweni yaweze kutumika,” alisema Sagini.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho, SACP Lazaro Mambosasa alisema licha ya Chuo hicho kuwa na maendeleo mazuri kitaaluma na ujenzi wa miundombinu, bado kinakabiliwa na changamoto ya kukosekana kwa miundombinu katika eneo jipya la mafunzo la mbinu za kivita lililopo Wilayani Kisarawe, Mkoa wa Pwani.
“Eneo hili ni muhimu sana kwa mafunzo kwa vitendo lakini halina miundombinu kwa mafunzo hayo kama vile mabweni ya wanafunzi, vyoo, mifumo yam aji safi na maji taka,” alisema Mambosasa.
Akizungumzia ziara yake katika Kikosi cha Mbwa na Farasi, Sagini alisema Kikosi hicho wana mbwa na farasi wenye uwezo mkubwa kutokana na mafunzo waliyopata, ila waorodheshe changamoto zao mbalimbali zikiwemo upungufu wa mbwa na ukosefu wa jengo la ofisi lenye ubora, wamuandikie Mkuu wa Jeshi hilo alafu zitafika Wizarani na kuzifanyia kazi.
“Mambo tunayo mengi sana lakini lazima tupange, na kupanga ni kuchagua, wachague vipengele vichache,vitatu mpaka vitano kwa miaka mitano hadi kumi ijayo, wayaandikie vizuri tujue mahitaji yao katika Kikosi hiki, hali iliyopo ni ipi, bajeti yake katika kutekeleza katika kufikia hali nzuri tunayoipenda, alafu wawasilishe kwa IGP na Wizara tuipate ili iweze kuingizwa katika mipango na bajeti kwa mwaka ujao,” alisema Sagini.
Naye Kamanda wa Kikosi hicho, SP Majura Kyariga, alimshukuru Naibu Waziri Sagini kwa kutembelea ofisi yake, na kuahidi kuyatekeleza maagizo yoye aliyoyatoa, pia alifurahia kwa kiongozi huyo kujua umuhimu wa mbwa na farasi katika kazi za ulinzi na usalama nchini.
“Mheshimiwa Naibu Waziri amejionea mwenyewe kazi mbalimbali tunazozifanya kwa kupambana na uhalifu kwa kutumia mbwa na farasi, ameweza kuona mbwa wanavyokamata, kutambua na kubaini silaha na nyara za Serikali pamoja na dawa za kulevya. Kwa umuhimu huo na jinsi nilivyomuambia tuna mbwa wachache, naamini Serikali itaweza kutuongezea mbwa ili tuongeze nguvu zaidi kupambana na wanaoingiza na kusafirsiha dawa za kulevya nje ya nchi, kulinda mipaka na katika viwanja vyetu vya ndege,” alisema SP Kyariga.