Na Dotto Mwaibale, Ikungi
MKUU wa Wilaya ya Ikungi, mkoani Singida, Jerry Muro, ameridhishwa na
kufurahishwa na mkandarasi wa kampuni ya M/S Chakwale Company Limited aliyekuwa
akijenga mradi wa maji wa Urafiki-Ikungi kwamba amefanya kazi hiyo kwa ufanisi
mkubwa sana.
Kufuatia hali hiyo, ameiagiza Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini
(RUWASA) kumlipa mkandarasi huyo fedha zilizobaki baada ya kukamilisha ujenzi
wa mradi huo ambao umegharimu zaidi ya Sh.Milioni 548.7.
Alitoa agizo hilo juzi wakati akiweka jiwe la msingi mradi wa maji ya bomba
wa Rafiki-Ikungi utakaohudumia kata mbili za Unyahati na Ikungi ambao umejengwa
kwa zaidi ya Sh. Milioni 548.7 ikiwa ni sehemu ya fedha za Uviko -19.
“Katika mradi huo hakuna hata shilingi iliyoliwa na hata ukiangalia
fedha aliyolipwa mkandarasi ni kidogo ukiangalia na thamani ya kazi
iliyofanyika, nitowe rai kwa RUWASA sasa tumalizane na mkandarasi,kazi yake ni
njema kabisa,” alisema.
Muro alisema baada ya kukamilika kwa mradi huo wananchi sasa waachane na
tabia ya kunywa maji ya mabondeni na mito badala yake watumie ya bomba ambayo
ni safi na salama.
Alisema serikai inatumia mamilioni ya fedha kujenga miradi hii ili
kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama.
“Tabia ya kwenda kunywa maji bondeni au mtoni kwa kisingizio mumeyazoea
yana radha nzuri iishe, tunywe maji ya bomba ili afya zetu ziwe nzuri, tuachane
na maji ya visima,” alisema.
Muro alisema serikali inawapenda wananchi wake hivyo inataka kuhakikisha
dhamira ya kumtua mama ndoo kichwani ambayo imekuwa ikisisitizwa na rais Samoa
Suluhu Hassan inatimia.
Alisema kukamilika mradi huu kutafanya upatikanaji wa huduma za maji katika
Wilaya ya Ikungi kufikia asilimia 57.3 na kwamba malengo ya serikali ni
kuhakikisha kiwango cha upatikanaji wa maji kinafikia asilimia 60 ifikapo
mwishoni mwa mwaka huu wa 2022.
Alisema serikali wikayani Ikungi imeshapitisha kwenye vikao vya Kamati ya
Maendeleo ya Wilaya (DCC) mpango wa uboreshaji wa usambazaji wa maji katika
tarafa ya Ikungi na maeneo mengine ambapo Ikungi sasa itaanza kuhudumiwa na
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Singida (SUWASA).
Muro alisema katika utekelezaji wa mradi huu hakuna hata shilingi moja
iliyoliwa na kuiagiza Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA)
kumlipa fedha zilizobaki Mkandarasi wa Kampuni ya M/S Chakwale Company Limited
ambaye amelipwa fedha za awali Sh.milioni 98.7 tu.
Aliongeza kuwa mradi huo katika awamu ya kwanza utakuwa na maeneo nane ya
umma ya kuchotea maji (vilula) na pia umetengenezwa ukiwa na uwezo wa kutoa
huduma ya kuwaunganisha wananchi maji majumba kutokana na miundombinu yake
kupita kwenye maeneo ya makazi ya watu.
Meneja Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa
Singida, Lucas Said, alisema ipo miradi tisa inayotekelezwa mkoani hapa kwa
fedha za Uviko-19.
Said alisema katika utekelezaji wa miradi hiyo mkoa wa Singida ulipewa
kiasi cha Sh.bilioni 4.
Kwa upande wake Kaimu Meneja Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini
(RUWASA), Wilaya ya Ikungi, Mhandisi Michael Ndunguru, alisema mradi huo umelenga
kuwahudumia wakazi 7500 wa eneo la makao makuu ya Wilaya ya Ikungi
linalojumuisha vijiji vya Ikungi na Muungano.
Ndunguru alisema kukamilika kwa mradi huu kutasaidia kupunguza maambukizi
ya magonjwa yatokanayo na ukosefu wa maji safi na salama na kusaidia wananchi
kufanya shughuli za kiuchumi na hivyo kuondokana na kero ya kutembea umbali
mrefu kutafuta maji.