Baadhi ya ofisi za madini zilizopo katika wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma ambazo zimewezesha kuongezeka kwa wanunuzi wa ndani na nje ya nchi.
Mchimbaji mdogo wa madini ya vito kutoka wilaya ya Tunduru Rashid Kanyunya kushoto,akithaminisha madini yake kwa Afisa madini wa wilaya ya Tunduru Shamia Sharifu kulia, ili kupata thamani halisi kabla ya kupeleka kwa sokoni.
Makamu mwenyekiti wa Chama cha wachimbaji wa madini ya vito na dhahabu mkoani Ruvuma(RUVREMA) Kassim Pazi wa kwanza kushoto waliokaa na afisa madini kutoka ofisi ya madini wilaya ya Tunduru Shamira Sharifu katikati,wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wachimbaji wadogo wa madini wa wilaya ya Tunduru.
Makamu mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini mkoani(RUVREMA)Kassim Pazi kulia,akizungumza na wanachama wa chama hicho Ndwela Msuya kushoto na mwingine ambaye hakufahamika jina lake juu ya umuhimu wa kushiriki kwenye zoezi la sensa ya watu na makazi linalotarajiwa kufanyika tarehe 23 nchini kote
Picha na Muhidin Amri
……………………….
Na Muhidin Amri,
Tunduru
WACHIMBAJI wadogo wa madini ya vito na dhahabu mkoani Ruvuma,wameiomba Serikali kupeleka elimu juu ya umuhimu wa sensa ya watu na makazi ili wachimbaji wote washiriki zoezi hilo kwa kutoa taarifa sahihi zitakazowezesha kufanikisha lengo la serikali.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wachimbaji hao walisema, kutokana na mazingira ya kazi zao ni vigumu kwa baadhi ya wachimba kushiriki vyema kwa kuwa bado hawajapa elimu yoyote kuhusu kuwepo kwa sensa na umuhimu wake.
Makamu mwenyekiti wa wachimbaji madini mkoa wa Ruvuma(Ruvrema) Kassim Pazi alisema,baadhi ya wachimbaji wanaishi na kufanya kazi kwenye maeneo magumu yasiofikika kwa urahisi na wengine hawajafika kwenye vijiji au mjini kwa zaidi ya miaka mitano kwa hiyo itakuwa vigumu kuwapata.
Kwa mujibu wa Pazi ni kwamba,njia pekee itakayowezesha wachimbaji wengi kushiriki sensa ya mwaka 2022 ni viongozi wa serikali na watu waliopewa dhamana ya kuratibu na kusimamia kazi hiyo, kwenda moja kwa moja katika maeneo ya machimbo ili kutoa elimu kabla ya siku iliyopangwa kufanyika kwa zoezi hilo.
Pazi alisema katika maeneo hayo hakuna mawasiliano yoyote, kwa hiyo ni vigumu baadhi yao kushiriki kwa kuwa wako kwenye machimbo kwa muda mrefu,hivyo sio rahisi kupata taarifa zozote na hadi sasa hawaelewi faida ya zoezi hilo na umuhimu wake.
Pazi ambaye pia ni makamu mwenyekiti wa kamati ya madini na viwanda nchini(Femata)alisema, sensa ni zoezi maalum lenye lengo la kupata idadi ya watu wote waliopo hapa nchini wakiwamo wachimbaji wa madini ili kupata taarifa muhimu zitakazowezesha kupanga mipango yake ya maendeleo.
Alisema, viongozi wa chama cha wachimbaji wilaya ya Tunduru na mkoa wako tayari kuisaidia serikali kufanikisha zoezi hilo, lakini hadi sasa serikali haijawashirikisha kama ilivyofanya kwa makundi mengine ya kijamii.
Alisema,matarajio ya wachimbaji katika sensa ya mwaka huu serikali kupitia wizara ya madini itaweka dodoso litakalosaidia kukusanya taarifa za wachimbaji wa madini ili kuweza kujua mahitaji yao na kuwahimiza wachimbaji wote kutoa ushirikiano na taarifa zao kwa usahihi.
Aidha,ameishukuru serikali kupitia wizara ya madini kwa uamuzi wa kujenga masoko ya madini mkoani Ruvuma ambayo yamewezesha wachimbaji wadogo hasa wa madini ya vito kupata sehemu ya uhakika na kuuza madini yao bila kudhurumiwa.
Mchimbaji wa madini kutoka wilaya ya Tunduru Ndwela Msuya,ameiomba serikali kuweka nguvu kubwa maeneo ya machimbo ili siku ya sensa ikiwezekana wachimbaji wakae sehemu moja ili makarani waweze kutekeleza majukumu yao na wachimbaji wapate nafasi ya kushiriki zoezi hilo muhimu kwa uchumi wa nchi yetu.
Msuya alisema,kama serikali haitajipanga vizuri na kutoyashirikisha baadhi ya makundi hasa yanayofanya shughuli zao kwenye maeneo magumu na yasio rasmi,kuna hatari ya kutowafikia watu wote siku ya sensa.
“naiomba serikali ituangalie sana sisi wachimbaji wadogo kwani tumesahaulika kwa muda mrefu sana, lazima itambue kuwa Tunduru kuna wachimbaji wengi wa madini ambao wako tayari kuhesabiwa katika sensa mwaka 2022”alisema Msuya.
Msuya,ameipongeza serikali kujenga masoko hayo ambayo yamesaidia sana wachimbaji wadogo kuuza madini yao kwa urahisi tofauti na siku za nyuma ambapo walilazimika kuuza kwa kutumia vipimi visivyo rasmi.
Alisema,kujengwa na kufunguliwa kwa masoko ya madini wilayani Tunduru, kumewezesha kuongezeka kwa wanunuzi wengi kutoka ndani na nje ya nchi na kuwataka wachimbaji wadogo kutumia masoko hayo kuuza madini badala ya kutumia masoko ya mitaani.
Mchimbaji Abdala Jumanne, amewaomba wachimbaji wenzake kushiriki zoezi hilo kwani ni jambo muhimu ili serikali iweze kupata idadi sahihi ya watu wake ili kuanisha mahitaji halisi ya wananchi yakiwamo makundi yenye
mahitaji maalum kama vile watu wenye ulemavu,watoto,wanawake na vijana.