Mkuu wa wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara Mariam Chaurembo akikabidhi vifaa mbalimbali vya michezo kwa mwanafunzi wa shule ya Sekondari Mkanona wilayani humu vilivyotolewa na Mbunge wa Jimbo la Nanyumbo Yahaya Mhata.
Mkuu wa wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara Mariam Chaurembo akimshukuru Mbunge wa Jimbo la Nanyumbo Mheshimiwa Yahaya Mhata kutokana na mchango wake katika kusaidia shughuli za maendeleo ikiwamo sekta ya michezo wilayani humo.
Mbunge wa Jimbo la Nanyumbu Yahaya Mhata,akizungumza na viongozi,walimu,wanafunzi na wazazi wa watoto wanaosoma katika shule ya Sekondari Mkanona kata ya Mkanona wilayani Nanyumbu.
Mkuu wa wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara Mariam Chaurembo kulia,akimpa hati maalum Mbunge wa Jimbo la Nanyumbu mkoani humo Mheshimiwa Yahaya Mhata kutokana na kutambua mchango wake katika suala zima la maendeleo katika wilaya hiyo.
…………………………..
Na Muhidin Amri,Nanyumbu
MKUU wa wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara Mariam Chaurembo,amewataka wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani humo, kushiriki katika michezo ili kuimarisha afya ya ubongo na kuwa na uwezo mzuri wa kufikiri na kufanya vizuri katika masomo yao.
Chaurembo amesema hayo jana wakati akikabidhi vifaa mbalimbali vya michezo kwa wanafunzi wa shule ya sekondari Mkanona Halmashauri ya Nanyumbu vilivyotolewa na Mbunge wa Jimbo la Nanyumbu Yahaya Mhata kwa lengo kuibua vipaji na kukuza michezo mashuleni.
Alisema,kwa kawaida binadamu anayeshiriki michezo anayo nafasi kubwa ya kufanya vizuri katika kutekeleza majukumu yake ya kila siku ikiwamo katika masomo darasani tofauti na asiyeshiriki michezo.
Amewahimiza wananchi wa Nanyumbu, kuwa na tabia ya kushiriki katika michezo mbalimbali na kufanya mazoezi ya mara kwa mara kwa ajili ya kuimarisha afya zao ili kuepuka uwezekano wa kupata magonjwa.
Aidha,amempongeza Mbunge wa Jimbo la Nanyumbu Yahaya Mhata kwa kutambua na kuthamini sekta ya michezo na kuongeza kuwa,vifaa hivyo vitawezesha kukuza sekta ya michezo katika wilaya hiyo.
Mbunge wa Jimbo la Nanyumbu Yahaya Mhata alisema,mkakati wake ni kuhakikisha vilabu na shule zote za msingi na sekondari vinapata vifaa ili kukuza vipaji ili kupata vijana wengi watakao liwakilisha Taifa letu.
Alisema,katika jimbo hilo kuna vijana wengi lakini wanashindwa kuonyesha na kuendeleza vipaji vyao kutokana na kukosa vifaa na kuwataka wadau kujitokeza kwa kusaidia sekta ya michezo katika jimbo la Nanyumbu.
Alisema, ni muhimu kwa vijana waliopo shuleni na hata wa mitaani kujikita katika michezo kwa kuwa michezo ni sehemu ya ajira na inasaidia sana kuimarisha afya za watu.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake Saleh Daimu,amemshukuru Mbunge huyo kwa msaada wa mipira na jezi na kuwaomba wadau mbalimbali kujitokeza kusaidia vifaa ili wanafunzi wengi wapate fursa ya kushiriki katika michezo.
Alisema, michezo ina faida kubwa kwa binadamu kama vile kutoa ajira kwa vijana, kuimarisha afya na kutoa fursa ya kufika maeneo mbalimbali.