VIJANA wa Klabu ya Wasaf Jogging ya Tunduru mjini wakiwa katika matembezi ya km 7 kwa ajili ya kuhamasisha wakazi wa wilaya hiyo kushiriki zoezi la sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika terehe 23 mwezi huu.
VIJANA kutoka kijiji cha Mtina wilayani Tunduru wakiwa na mabango yenye ujumbe wa kuwataka Watanzania kujiandaa kushiriki katika zoezi la sensa ya watu na makazi.
Baadhi ya vijana wanaojishughulisha na biashara ya boda boda Tunduru mjini wakiwa na mabango ya kuhamasisha watu kujiandaa kushiriki sensa.
Mkuu wa wilaya ya Tunduru Wakili Julius Mtatiro kulia na baadhi ya viongozi wa wilaya hiyo wakiondoa kitambaa kuashiria uzinduzi rasmi wa Bonanza maarufu la Samia Sensa Bonanza-Tunduru linalolenga kuhamasisha wakazi wa wilaya hiyo na Watanzania kushiriki katika zoezi la sensa ya watu na makazi linalotarajiwa kufanyika mwezi huu.
vijana kutoka maeneo mbalimbali katika wilaya ya Tunduru wakiwa na mabango yenye ujumbe wa kuhaamasisha Watanzania kujiandaa kushiriki zoezi la sensa ya watu na makazi.
Mkuu wa wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro kushoto,akimtambulisha mchezaji wa Timu ya Geita Gold inayoshiriki Ligi kuu ya NBC Ditram Nchimbi katikati na mwanamuziki wa kizazi kipya Frank Ngumbuchi(FOBI)ambao watakuwa sehemu ya wahamasishaji wa zoezi muhimu la sensa ya watu na makazi katika wilaya hiyo mara baada ya mechi ya hiari wa mpira wa miguu kati ya Timu Ditram na Timu Fobi ambapo Timu Fobi ilifungwa goli 1-0 goli lililofungwa na Ditram Nchimbi dk 80.
Kikosi cha Timu Fobi
Kikosi cha Timu Fobi
Wachezaji wa Timu Fobi na Timu Ditram wakigombea mpira wakati wa mechi ya hiari kati ya timu hizo iliyofanyika katika uwanja wa CCM Tunduru mjini kwa lengo la kuhamasisha wakazi wa wilaya ya Tunduru na Watanzania kwa ujumla kushiriki katika zoezi la sensa ya watu na makazi tarehe 23 Mwezi huu.
…………………………………
Na Muhidin Amri,
Tunduru
WAKAZI wa Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma,wameshiriki katika Bonanza maalum la kuhamasisha wananchi wa wilaya hiyo na Watanzania kujiandaa kushiriki kikamilifu zoezi la sensa ya watu na makazi linalotarajiwa kufanyika tarehe 23 mwezi huu nchini kote.
Bonanza hilo maarufu kwa jina la SAMIA SENSA BONANZA-TUNDURU limeshirikisha michezo mbalimbali ya matembezi ya hiari umbali wa km 7,mpira wa miguu,bao,drafti,mpira wa wavu,kukimbiza kuku na rede kwa wasichana ambapo washiriki wametoka kata zote 39 za wilaya ya Tunduru.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Bonanza hilo Mkuu wa wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro,amewataka wananchi kujiandaa kushiriki kikamilifu katika zoezi la sensa na makazi ili kuiwezesha serikali kupanga maendeleo,kupunguza umaskini na kukuza uchumi wa nchi yetu.
“matokeo ya sensa ya mwaka huu itasaidia serikali kupata taarifa na takwimu sahihi za wananchi wake na kupanga mipango ya maendeleo hasa ikizingatiwa kuwa, katika sensa ya mwaka 2012 wilaya yetu haikufanya vizuri kutokana na baadhi ya wananchi kutoshiriki zoezi hilo muhimu”alisema.
Amewaomba Wananchi, kutoe ushirikiano kwa watu waliopewa kazi ya kukusanya takwimu na taarifa mbalimbali ili zoezi hilo liweze kufanikiwa kama ilivyopangwa na Serikali.
Mtatiro ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya usalama amewataka viongozi wa ngazi mbalimbali wilayani humo, kuendelea kutoa elimu ya umuhimu wa sensa kwa wananchi ili kuwaweka tayari kushiriki zoezi hili muhimu kwa maendeleo ya nchi.
Amewashukuru wakazi wa Tunduru hasa vijana na watu wengine waliofika kushuhudia Bonanza la Samia Sensa-Tunduru lililofanyika katika uwanja wa michezo wa CCM Tunduru mjini kuacha shughuli zao na kushiriki katika Bonanza hilo.
Kwa mujibu wa Mtatiro,Bonanza hilo ni mwanzo wa kuanza kwa Ligi ya Samia Sensa Bonanza-Tunduru ambayo itafanyika kuanzia ngazi ya vijiji,kata,tarafa na baadaye ngazi ya wilaya ambayo itatumika kwa kuhamasisha wananchi kushiriki zoezi la Sensa ya watu na makazi pamoja na kuibua vipaji kwa vijana wa wilaya hiyo.
Aidha katika Bonanza hilo, kulifanyika mechi ya hiari ya mpira wa miguu kati ya Timu Ditram Nchimbi na Timu ya mwanamuziki wa kizazi kipya Frank Ngumbuchi(FOBI) na Timu Ditram iliifunga Timu Fobi goli 1-0. goli lililofungwa na Ditram Nchimbi dk 80.
Kwa upande wake Ditram Nchimbi,amewaomba Watanzania kujiandaa kushiriki kikamilifu katika zoezi la sensa ya watu na makazi na kuwataka wana michezo na makundi mengine kuungana na Serikali kuhamasisha wananchi kushiriki katika zoezi hilo.
Alisema,sensa ya watu na makazi ni muhimu sana kwani serikali ina lengo la kupata taarifa sahihi za idadi ya watu wake ili iweze kupanga mipango na kutoa hudumu za kijamii.
Naye Nahodha wa Timu ya Fobi Frank Ngumbuchi(Fobi)alisema ataendelea kuiunga mkono serikali katika kufanikisha utekelezaji wa zoezi la sensa na kuwaomba wakazi wa Tunduru na mkoa wa Ruvuma kuhakikisha kila mmoja anahesabiwa ili serikali iweze kupata takwimu sahihi na za uhakika wakati wa kupanga mipango ya maendeleo.