Mkuu wa Mkoa wa Tabora akiongea na waandishi wa Habari hawapo pichani kwenye ukumbi ndogo wa Katibu Tawala mkoa was Tabora
…………………………………………
WADAU wa sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi na wafanyabiashara kutoka Mikoa ya Kigoma na Tabora wametakiwa kuchangamkia fursa zilipo kwenye maonesho ya nane nane mwaka huu pamoja na kujionea teknolojia mpya zinazotumika kuongeza thamani.
Wito huo umetolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt Batilda Burian alipokuwa akiongea na vyombo vya habari ofisini kwake kuhusiano na ujio wa maonesho ya nane nane ambayo yanaanza leo Agosti 1 hadi Agosti 8.
Alisema maonesho ya mwaka huu yameongezewa ubunifu mkubwa kwani washiriki wote wakiwemo wakulima, wafugaji, wavuvi, taasisi na wadau mbalimbali watapata fursa ya kujifunza teknolojia mpya zitakazosaidia kuongeza uzalishaji wenye tija.
Aliongeza kuwa hiyo ni fursa muhimu ya kutangaza bidhaa za kilimo, mifugo na uvuvi zinazozalishwa na wadau mbalimbali ikiwemo kuunganishwa na mtandao wa masoko ya ndani na nje ya nchi.
Balozi Batilda alibainisha lengo la maonesho hayo kuwa ni kusambaza teknolojia bora za kilimo, mifugo na uvuvi kwa wakulima, wafugaji na wavuvi ili kufanya shughuli hizo kuwa endelevu, kuwa na masoko ya uhakika, kuongeza thamani na kukuza biashara zao.
‘Serikali imeamua kuyafanya maonesho haya kuwa endelevu na Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Sekretarieti za Mikoa wataanzisha Vituo vya Mafunzo kwa Wakulima na Vituo hivyo vitakuwa atamizi (incubate) kwa wakulima na wafugaji’, alisema.
Aidha vituo hivyo vitaendelea kutoa mafunzo kwa kwa kipindi cha mwaka mzima na wakati huo huo kuwa sehemu ya kuzalisha mazao ya kilimo kwa kuwa sehemu zote za maonesho zina mashamba madogo na makubwa.
Alitaja walengwa wakuu katika maadhimisho hayo kuwa ni wakulima, wafugaji, wavuvi, wasindikaji, wafanya biashara, wajasiriamali na wadau wote wanaohusika katika mnyororo wa thamani ikiwemo maliasili, ufugaji nyuki na biashara ya mazao.
Taasisi nyingine zitakazoshiriki maonesho hayo ya Kanda ya Magharibi yatakayofanyika katika uwanja wa Nane Nane-Ipuli Mjini Tabora ni za fedha, Wakala za Serikali, Vyama vya Ushirika, Mashirika yasiyokuwa ya kiserikali na sekta binafsi.
Akitoa wito kwa niaba yake na kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma aliwataka wananchi wote na wadau mbalimbali kujitokeza kwa wingi kushiriki katika maonesho hayo ili kujionea teknolojia mpya zilizopo, kujifunza na kutangaza fursa mbali mbali zilizopo katika Mikoa hiyo 2 ya Tabora na Kigoma.