***********************
Na Mwandishi wetu, Mirerani
OFISI ya Afisa madini mkazi Mkoa wa kimadini (RMO) wa Mirerani, imelenga kukusanya shilling ibilini 7.4 baada ya kukusanya shilingi bilini 2.3 kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022 sawa na asilimia 77.41 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 3.
Afisa madini mkazi RMO Fabiani Mshai ameyasema hayo wakati akisoma taarifa ya utendaji kazi kwa mwaka jana, mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara.
Hata hivyo, RMO Mshai amesema kwa mwaka huu wa fedha 2022/2023 wameweka lengo la kukusanya shilingi bilioni 7.4, kupitia ukusanyaji wa uzalishaji wa madini ya eneo hilo.
Amesema ofisi ya madini Mirerani ina watumishi 28 wa kudumu wa kada za jiolojia, uhandisi migodi, mazingira, uhasibu na ufundi sanifu na watumishi watano wa mikataba wa ukaguzi wa madini ya ujenzi.
Amesema shughuli zinazofanywa na ofisi hiyo ni udhibiti wa uzalishaji madini, ukusanyaji maduhuli ya serikali ikiwemo mrabaha, ada za ukaguzi na kuhamasisha uhifadhi wa mazingira.
“Pia uthaminishaji wa madini, utoaji wa leseni za uchimbaji na biashara ya madini inayojumuisha usimamizi wa masoko ya madini na utoaji wa vibali vya usafirishaji madini ndani na nje ya nchi,” amesema RMO Mshai.
Amesema kwenye soko la madini ya Tanzanite lenye majengo manne ikiwemo benki ya NMB, Sadiki Mneney, Erasto Msuya na Paul Mollel ambapo kuna wanunuzi wakubwa 55.
Kaimu mkuu wa wilaya ya Simanjiro, Mbaraka Batenga amewataka wajumbe wa kamati ya eneo tengefu la Mirerani kumpa ushirikiano wa kutosha RMO Mshai ili lengo la kukusanya sh7.4 bilioni lifanikiwe.
“Yeye hana mgodi wala siyo maagizo yake binafsi, hapana ni maagizo ya serikali kuhakikisha fedha hizo zinakusanywa kupitia madini yanayopatikana na lengo litafanikiwa endapo mtashirikiana,” amesema Batenga.