Mratibu wa Sensa Mkoa wa Singida, Naing’oya Kipuyo, akizungumza na Wakufunzi wa Makarani wa Sensa ya Watu na Makazi baada ya kuhitimu mafunzo hivi karibuni yaliyofanyika Chuo cha Ufundi VETA mkoani hapa.
Na Abby Nkungu, Singida
WAZAZI wa watoto wenye ulemavu wametakiwa kuhakikisha kuwa kundi hilo
linahesabiwa wakati wa Sensa ya Watu na Makazi ili kuiwezesha Serikali kupata
takwimu sahihi kwa ajili ya kuandaa mipango ya kibajeti, Sera, Sheria, Kanuni
na Programu zitakazojibu changamoto zao.
Mwito huo ulitolewa na Mratibu
wa Sensa ya watu
na Makazi mkoa wa Singida, Naing’oya Kipuyo wakati akizungumzia
maandalizi ya zoezi hilo lililopangwa kufanyika kote nchini Agosti 23, mwaka
huu.
Alisema kuwa wakati Serikali ikitekeleza Programu Jumuishi ya Taifa ya
miaka mitano juu ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto iliyoanza
mwaka jana, takwimu sahihi za kundi hilo ni muhimu sana katika kufanikisha
mipango mbalimbali ya watoto iliyowekwa.
“Programu hii inashughulika na masuala mtambuka ya watoto kuanzia umri wa
miaka 0 hadi 8; wakiwemo watoto wenye ulemavu na wenye mahitaji maalum, hivyo
ni muhimu kwa wazazi na walezi wao kuhakikisha wanahesabiwa na kueleza bayana
bila kificho hali zao” alisisiza Kipuyo.
Alisema kuwa ni vyema wazazi na walezi wakatambua kuwa zoezi la sensa ya watu na
makazi linafanyika kwa mujibu wa Sheria ya takwimu sura 351, hivyo iwapo mtu
atamficha mtoto wake au yeye mwenyewe kukataa kuhesabiwa anaweza kushitakiwa chini
ya kifungu 6 (2) a cha sheria hiyo.
Alisema, kwa upande wake Serikali imejipanga vizuri ili kuhakikisha kuwa
zoezi hilo muhimu kwa Taifa linafanikiwa bila kikwazo chochote kwa kuunda
kamati za sensa hadi ngazi ya kitongoji na mitaa kwa ajili ya kutoa elimu na
hamasa ili kila mwananchi aweze kujitokeza kuhesabiwa.
Hata hivyo, mmoja wa wazazi Patrick Mdachi mkazi wa Mitunduruni Manispaa ya
Singida alisema kuwa pamoja na
maandalizi mazuri yaliyofanyika, bado kuna haja ya elimu na hamasa zaidi
ili kuondoa dhana na imani potofu
kwa baadhi ya jamii juu ya watoto wenye
ulemavu katika kuhesabiwa.
“Mpaka sasa bado shule zenye watoto wenye mahitaji maalum zinapata
changamoto kubwa kupata wanafunzi, baadhi wanafichwa majumbani na wengine wanaandikishwa wakiwa na umri mkubwa.
Ipo haja ya elimu na hamasa zaidi kwa kutumia wazee wa mila, viongozi wa dini,
vitongoji, mitaa na wengine wenye ushawishi” alieleza.
Kauli ya Mdachi inaungwa mkono na Mwalimu wa kitengo cha Elimu Maalum shule
ya msingi Mchanganyiko Mgori katika halmashauri ya wilaya ya Singida, Hemed
Kilango ambaye anasema wazazi wengi wenye watoto walio na mahitaji maalum
wamekuwa wakisita kuwapeleka watoto wao shule kwa kuhofia watateseka zaidi
kutokana na kukosekana miundombinu ya kutosha huko.
“Kama wanawaficha kwenda shule, ni dhahiri hata sensa wanaweza
kuwaficha, hivyo ni lazima wazazi na
walezi wakaelimishwa ipasavyo ili watambue kuwa mipango ya vifaa vya kutosha
kujifunzia na kufundishia na miundombinu rafiki kwa watoto wenye ulemavu
inategemea sana takwimu sahihi za sensa” alifafanua Mtaalamu huyo wa elimu
maalum.
Naye, Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Tumaini Viziwi ya mjini Singida,
Francis Edward alieleza kuwa wamekuwa wakipokea idadi ndogo ya wanafunzi
kutokana na wazazi kuwaficha watoto wenye mahitaji maalum wakidhani kwa kufanya
hivyo watajiaibisha au kujifedhehesha.
Kulingana na ratiba ya maandalizi ya zoezi hilo, mafunzo ya wakufunzi wa
sensa ngazi ya mkoa Singida
yamehitimishwa juzi ambapo yatafuatiwa na mafunzo mengine katika halmashauri
zote saba hapo kesho
yatakayohusisha makarani na wasimamizi
zaidi ya 15,400.