Waziri wa Maji Juma Hamid Aweso (wa tatu kushoto) akikaribishwa na Mkuu wa Wilaya ya Sikonge John Pallingo (aliyeshika kipaza sauti) ili kuzungumza na wakazi wa kijiji cha Utyatya, kata ya Kisanga Wilayani Sikonge Mkoani Tabora alipofanya ziara ya siku moja kukagua Bwawa la Maji la Utyatya.
……………………………………..
Na Lucas Raphael,Tabora
Wasimamizi wa Mabonde ya maji nchini wametakiwa kuhakikisha jamii inakuwa na uelewa mpana wa kutunza vyanzo vya maji ili ishiriki kikamilifu kulinda vyanzo hivyo.
Rai hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Maji Jumaa Aweso alipokuwa akizungumza na wakazi wa kijiji cha Utyatya, kata ya Kisanga Wilayani Sikonge Mkoani Tabora alipofanya ziara ya siku moja kukagua Bwawa la Maji la Utyatya.
Alisema Bwawa hilo ambalo ni chanzo kikuu cha maji ya kunywa kwa wakazi wa Mji wa Sikonge na baadhi ya kata kinapaswa kulindwa na kutunzwa ipasavyo ili kiendelee kunufaisha wananchi.
Alisisitiza kuwa ni jukumu la Wizara hiyo kuhakikisha vyanzo vya maji vyote vinalindwa, kutunzwa na kuendelezwa hivyo akawataka Maofisa wa Bonde kutekeleza wajibu wao ipasavyo.
‘Maofisa Bonde badilikeni, acheni kukaa maofisini tu, nendeni mkakague mabonde yote, shirikisheni jamii mipango yenu, waelimisheni umuhimu wa kutunza vyanzo vya maji, msisubiri hadi wavamie na kuanza kulima’, alisema.
Waziri Aweso alibainisha kuwa mabonde yote 9 yaliyopo hapa nchini ni vyanzo muhimu sana kama vitapewa uangalizi wa karibu, aliwataka Maofisa hao kukaa na wakulima na wafugaji wanaoshi karibu na vyanzo hivyo na kuwapa elimu.
Alisisitiza kuwa serikali imetoa vitendea kazi vya kutosha hivyo hakuna sababu kwa Maofisa hao kushindwa kutembelea vyanzo vya maji, alishauri warsha au semina zao zifanyikie katika maeneo hayo ili kuongeza uelewa kwa jamii.
Alieleza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amedhamiria kumtua mama wa Sikonge ndoo kichwani, ndio maana ameleta fedha nyingi kwa ajili ya kuboreshwa bwawa hilo, hataki kusikia wala kuona akinamama wakihangaika kwa kukosa maji.
Aidha ili kuhakikisha mabonde ya maji yanakuwa na nguvu kubwa na kutimiza majukumu yao ya kila siku ipasavyo ya kulinda na kuboresha mazingira ya mabonde hayo alishauri kuanzishwa kwa Jumuia za watumaiji Maji.
Mkurugenzi wa Rasilimali wa Maji Nchini Mhaidrolojia George Lugomela alieleza kuwa serikali imletea kiasi cha sh mil 200 kwa ajili ya kulifanyia maboresho makubwa bwawa hilo.
Alitaja baadhi ya shughuli zitakazofayika kuwa ni kuzungusha nguzo katika mipaka yote ya bonde hilio ikiwemo kuboresha uoto wa asili,kujenga mabirika ya kunyweshea mifugo, kung’oa magugu maji na kuboresha utoto wa maji.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Bonde la Maji la Ziwa Tanganyika Mhaidrolojia Julius Shilungushela alishukuru serikali kwa kuwaletea fedha za kukarabati bwawa hilo na kushauri kina kiongezwe na jamii ishirikishwe katika mipango yote.