Dar es Salaam
Vijana balehe kote nchini wameungana na viongozi wa dini, wafanyabiashara,vyama vya kiraia, wanamichezo, waandishi wa habari, UNICEF na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa kuzindua kampeni ya BINTI, inayolenga kukomesha ndoa za utotoni nchini. Kampeni hiyo pia inakusudia kuhamasisha umma kushinikiza mabadiliko ya sheria ya ndoa ili kuongeza umri wa mtoto wa kike kuingia kwenye ndoa na kubadili mitazamo ya jamii kuhusu umuhimu wa mtoto wa kike.
“Huu ndiyo wakati wa kutatua mila, desturi na kanuni za kijamii zinazotukwamisha katika kutimiza ndoto za maisha yetu,” alisema Nancy Kasembo (17), mwenyeji wa mkoa wa Shinyaga na Mwenyekiti wa Baraza la Watoto la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (JCURT). “Kama vijana, yatupasa kuifanya Tanzania kuwa mahali ambako kila mtoto anapendwa, analindwa, na haki zake zinastawi,” alisisitiza Nancy.
BINTI ni wito wa kuchukua hatua. Kampeni Inawahimiza wazazi na jamii kuchelewesha ndoa za binti zao walio na umri wa chini ya miaka 18 na kuwasaidia wasichana kuendelea na masomo ya elimu ya sekondari ili kupata maarifa na stadi zitakazowaandaa kwa maisha yenye ustawi katika siku za baadaye na kusaidia kukabiliana na ukosefu wa usawa wa jinsia.
“Kuna madhara si tu kwa mtoto wa kike na si tu kwa wanawake, bali kwa taifa. Ninatoa wito kwamba tumalize ndoa za utotoni kwa sababu ya madhara yake—maisha ya msichana yanaharibiwa kabisa,” alisema Askofu Dkt. Stanley Hotayi, wa Kanisa la Anglikana, Jimbo la Arusha na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Baraza la Kikristo Tanzania (CCT). Askofu Dkt. Hotayi aliongeza kuasa akisema: “Ndugu zangu Watanzania, huu ni wajibu wa kila mmoja kutekeleza jambo hili, na si la mtu mmoja. Kwa kushirikiana pamoja tutakomesha ndoa za utotoni.”
Inakadiriwa kwamba wanawake 3 kati ya 10 nchini Tanzania waliingia kwenye ndoa wakiwa wangali watoto (wakiwa na umri wa chini ya miaka 18), jambo linaloifanya Tanzania kuwa nchi ya 11 duniani yenye mabibi harusi watoto.
“Suala la ndoa za utotoni nchini Tanzania limechelewa kufanyiwa mabadiliko. Na katika jambo hili kuna mambo mawili, kwanza ni Sheria ya Ndoa ambayo inahitaji marekebisho, pili ni mazoea ya jambo hili kufanyika katika jamii yetu. Si suala jepesi kwa sababu kuna vichocheo vingi vinavyosukuma familia kuingia katika ndoa za utotoni, moja wapo ni umaskini. Lakini, tunaweza kuzuia. Hatuna budi kuendelea kushinikiza hadi sheria ibadilishwe na hadi taratibu hizo na vichocheo vibadilike,” alisema Rebeca Gyumi, mkurugenzi mtendaji wa shirika la Msichana Initiative.
Hatua kubwa kwa kampeni ya BINTI ni utiaji saini ahadi ya kusaidia kuzuia ndoa za utotoni katika familia na jamii kwa kuacha kushiriki katika kuziendeleza. AHADI HII ni rahisi lakini ina nguvu kubwa katika mtandao, nje ya mtandao, kupitia ujumbe mfupi wa simu, a U-Report na inaweza kutumwa katika mitandao ya kijamii, yote ikiwa ni hatua ya kuunga mkono jitihada za kumaliza ndoa za utotoni nchini Tanzania.
“Tuna deni kwa kila mtoto wa Kitanzania, bila kujali ni wa jinsi gani, haki ya kupata elimu, afya, na ulinzi, na kwa kuwa kampeni hii inalenga kuhamasisha hatua ili kumaliza ndoa za utotoni nchini mwetu kwa hakika inakaribishwa na imekuja wakati sahihi,” alisema Sophia Byanaku, Mwanzilishi Mwenza wa Doctors Plaza Poly Clinic na mhamasishaji.
Tanzania ambayo takwimu zinaonyesha kuwa ina idadi ya watu milioni 60, miongoni mwao asilimia 50 ni wenye umri wa chini ya miaka 18, inazidi kukabiliwa na majukumu makubwa ya kutoa elimu bora, kuimarisha huduma za afya, na changamoto ya ajira kwa vijana, pamoja na vikwazo vingine vingi vilivyopo.
“Yatupasa kutazama kwa makini fursa ambazo watoto wa kike wanazikosa nchini Tanzania kwa sababu ya ndoa za utotoni,” alisema Shalini Bahuguna, Mwakilishi wa UNICEF nchini Tanzania. “Pale wasichana wanapowekewa mazingira ya kutarajia kupoteza elimu yao, utoto wao na ndoto zao ili waoelewe, ni jambo linalodhuru afya yao ya akili, na wanawekwa katika hatari ya kukumbwa na ukatili kila siku, unyonyaji, changamoto za kiafya na umaskini. Hawawezi kutimiza vipawa vyao na kutoa mchango wa maana katika jamii.”
Kuzuia ndoa za utotoni ndiyo msingi mkuu wa kukabiliana na masuala yanayowahusu watoto na vijana na maisha ya fursa, thamani ya wasichana katika jamii, kuvunja umaskini wa kurithishwa kutoka kizazi hadi kizazi, na kuhakikisha kwamba vijana wanakuwa mawakala wa kuleta mabadiliko chanya.
“Kama ningeolewa wakati nikiwa bado mtoto, hakuna namna ambayo ningefanya ili kupata fursa zote ambazo nimezipata hadi sasa. Kama kijana wa Kitanzania, ambaye nina bahati ya kufanya yale ninayofanya, nashindwa kuwaza maumivu makali na huzuni ambayo wasichana wengi wanapitia hivi sasa, wakiwa wamekwama kwenye ndoa kama watoto. Hii si sawa. Wasichana wanapaswa kuwa wakicheza na rafiki zao, wamalize shule, na kujijengea majina yao na kulijenga taifa letu hili kubwa,” alisema Meena Ally, mtangazaji wa redio na mhamasishaji.
“Kama mcheza kandanda, najua kwamba isingaliwezekana kwa mimi kufuatilia na kutimiza ndoto zangu kama ningeolewa nikiwa mtoto. Ninataka kila msichana nchini Tanzania apate fursa sawa kama mimi nilivyopata, kutimiza ndoto zao pasipo na hofu ya ndoa za utotoni,” alisema Zaiyonce Karabani, mcheza soka wa timu ya Fountain Gate Princess.
Binti, ni kampeni isiyo na mipaka iliyobuniwa ili kuwashirikisha watu wote nchini Tanzania ili waweke AHADI ya kukomesha ndoa za utotoni kwa kutoshiriki katika ndoa hizo za watoto. Binti ni mhusika wa kufikirika anayewakilisha mabinti zetu wote nchini Tanzania, ambao wanataka kukua na kufikia vipawa vyao kikamilifu.
“Ni muhimu tuchukue msimamo sasa kwa ajili ya kila msichana nchini Tanzania. Kila mtu ana kitu cha kutoa ili kuendeleza vita hivi: serikali, vyama vya kiraia, viongozi wa dini, familia, na jamii kwa ujumla. Hivi haviwezi kuwa vita vya msichana au mwanamke mmojammoja peke yake. Vinapaswa kuwa vita vya kila mmoja, hasa wanaume—baba, kaka, na watoto wetu wa kiume ili kusukuma ajenda dhidi ya ndoa za utotoni na masimulizi yaliyofubaa,” alisema Doris Mollel, Mwanzilishi wa Taasisi ya Dorris Mollel.