Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kuanzia tarehe Julai 21, 2022 lilifanya Misako na doria katika maeneo mbalimbali ya Mkoa dhidi ya wahalifu wa matukio ya uvunjaji wa nyumba na maduka usiku na mchana na kuiba. Katika Misako hiyo jumla ya watuhumiwa 13 wa matukio ya uvunjaji na kuiba walikamatwa, wahamiaji haramu 14 raia wa nchini Rwanda walikamatwa. Aidha katika Misako hiyo mali mbalimbali za wizi zilikamatwa toka kwa watuhumiwa na baadhi zimeanza kutambuliwa na wahanga katika vituo vya Polisi “Central Mbeya”, Kituo cha Polisi Mbalizi na Kituo cha Polisi Rujewa Wilayani Mbarali.
KUKAMATWA KWA WATUHUMIWA WA KUJIHUSISHA NA VITENDO VYA KIHALIFU.
Mnamo tarehe 24.07.2022 majira ya saa 08:00 usiku, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kufuatia taarifa za kiintelijensia lilifanya msako dhidi ya wahalifu wa matukio ya kuvunja nyumba usiku na kuiba huko Iyunga na maeneo mbalimbali ya mji mdogo wa Mbalizi.
Katika msako huo, jumla ya watuhumiwa 08 wa matukio ya kuvunja na kuiba walikamatwa ambao ni:-
- ELIA NGOVULE [22] Mkazi wa Mbalizi.
- LISBON GEORGE [27] Mkazi wa Uyole.
- ELIA RUBEN [21] Mkazi wa Mbalizi.
- OFRENI MWAKIPESILE [35] Mkazi wa Mbalizi.
- JIBU MUMBA [24] Mkazi wa Mbalizi.
- VICTOR SANKE [22] Mkazi wa Iyunga.
- DENIS JOSEPH [22] Mkazi wa Iyunga.
- FURAHA KANDONGA [35] Mkazi wa Mbalizi.
Watuhumiwa wamekiri kujihusisha na matukio ya uvunjaji na kuiba nyakati za usiku na mchana katika Mji Mdogo wa Mbalizi na maeneo ya Iwambi na Iyunga Jijini Mbeya. Watuhumiwa wote wanaendelea kuhojiwa na pindi upelelezi utakapokamilika watafikishwa Mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.
Sambamba na hilo katika muendelezo wa Misako dhidi ya wahalifu wa matukio ya kuvunja nyumba na kuiba, mnamo tarehe 21.07.2022 Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya msako huko maeneo ya Iduda na Nsoho Jijini Mbeya na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa 02 wa matukio ya kuvunja nyumba mchana na kuiba hasa maeneo ya nyumba za walimu wa Shule ya Sekondari Loleza iliyopo Jijini Mbeya.
Watuhumiwa waliokamatwa ni:-
- RAJABU RICHARD [21] Mkazi wa Nsoho.
- TUMAINI NELSON [18] Mkazi wa Nsoho.
Watuhumiwa wamepekuliwa katika makazi yao kwa mujibu wa sheria na kukutwa na mali za wizi ambazo ni simu mbili za mkononi na radio moja. Upelelezi wa shauri hili unaendelea na mara baada ya kukamilika watafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.
KUKAMATWA KWA MTUHUMIWA WA KUVUNJA DUKA USIKU NA KUIBA.
Mnamo tarehe 25.07.2022 majira ya saa 11:30 jioni huko Kijiji cha Igava, Kata ya Mawindi, Tarafa ya Rujewa, Wilaya ya Mbarali, Mkoa wa Mbeya. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya msako na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa wa muda mrefu mwenye tuhuma za kujihusisha na matukio mbalimbali ya uvunjaji aitwaye SAMATO MBASHA [35] Mkazi wa Igava, Mlinzi wa Soko akiwa na bidhaa mbalimbali alizoiba kwa watu tofauti na nyakati tofauti.
Katika upekuzi uliofanywa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa mujibu wa sheria kwenye makazi ya mtuhumiwa, alikutwa na mali mbalimbali za wizi ambazo ni:-
- Baiskeli 06,
- Kompyuta 02,
- TV Flat screen 03,
- Viti vya Plastiki 08,
- Speaker 03,
- Radio Subwoofer 03,
- Radio ndogo 02,
- Mitungi ya Gesi 02,
- Birika la umeme 01,
- Cherehani 01,
- Begi 01 lenye nguo mbalimbali,
- Mashine za kunyolea nywele 02,
- Ngazi ya chuma 01,
- Mzani 01,
- Vifaa mbalimbali vya umeme,
- Betri ya gari 01,
- Stuli ndefu ya bar,
- Msumeno na vifaa mbalimbali vya kuvunjia nyumba na maduka.
Mtuhumiwa ameeleza kuwa majira ya usiku akiwa kazini kama mlinzi hutumia muda huo kuvunja maduka na kuiba. Baada ya mahojiano mtuhumiwa amekiri kutenda matukio hayo na kutaja baadhi ya wafanyabiashara aliowaibia. Baadhi ya Wahanga wamezitambua mali zao. Mtuhumiwa atafikishwa mahakamani mara upeleelzi utapokamilika.
KUKAMATWA KWA MTUHUMIWA WA KUVUNJA USIKU NA KUIBA.
Mnamo tarehe 24.07.2022 majira ya saa 05:30 usiku huko Mtaa wa Mtakuja, Kata ya Usongwe, Tarafa ya Usongwe, Wilaya ya Mbeya Vijijini na Mkoa wa Mbeya. Askari Polisi wakiwa katika msako walimkamata FREDY HALE [18] Mkazi wa DDC – Mbalizi anayejihusisha na makosa ya uvunjaji wa nyumba na kuiba TV, Radio na vyombo vya ndani.
Mtuhumiwa alihojiwa na kukiri kujihusisha na matukio hayo ambapo alieleza kuwa alivunja nyumba ya CLERINA ZAKARIA na kuiba ndoo mbalimbali za Mhanga na baadae alipekuliwa na kukutwa na ndoo hizo. Mtuhumiwa atafikishwa Mahakamani mara baada ya Upelelezi kukamilika.
KUKAMATWA KWA MTUHUMIWA WA KUVUNJA NYUMBA USIKU NA KUIBA.
Mnamo tarehe 24.07.2022 majira ya saa 10:00 jioni huko Maeneo na Kata ya Ilomba, Tarafa ya Iyunga, Jiji na Mkoa wa Mbeya. Askari Polisi walifanya msako na kufanikiwa kumkamta HERMAN MLYUKA [29] Mkazi wa Ilomba kwa kosa la kuvunja nyumba usiku ya VICTORIA NGIMBA na kisha kuiba kitanda cha chuma kimoja, magodoro 02, Neti 01, TV Flat Screen 01 aina ya Samsung inchi 32 pamoja na radio moja Sub-Woofer aina ya Home base.
Baada ya kumuhoji amekiri kuhusika na tukio hilo na alipopekuliwa katika makazi yake kwa mujibu wa sheria alikutwa na Kitanda kimoja cha chuma, magodoro mawili na Neti vyote vimetambuliwa na Mhanga. Mtuhumiwa atafikishwa Mahakamani mara Upeleezi utapokamilika.
KUPATIKANA NA BHANGI.
Mnamo tarehe 24.07.2022 majira ya saa 06:30 mchana, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya msako huko Kizuizi cha Kijiji cha Kayuki, Kata ya Ilima, Tarafa ya Pakati, Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Mbeya na kufanikiwa kumkamata NEEMA BUKUKU [34] Mkazi wa Gombe – Uyole Mbeya akiwa na bhangi kiasi cha debe 03 sawa na uzito wa Kilogramu 13 ndani ya mifuko ya salfeti akiwa ndani ya gari aina ya Coaster akitokea Kyela kwenda Mbeya. Mtuhumiwa ni muuzaji na atafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.
KUINGIA NCHINI BILA KIBALI.
Mnamo tarehe 24.07.2022 majira ya saa 01:45 jioni huko Kizuizi cha Polisi Chalangwa kilichopo Kata ya Chalangwa, Tarafa ya Kiwanja, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya. Askari Polisi wakiwa doria walifanikiwa kuwakamata Wahamiaji haramu 14 kati yao wanaume 11 na mwanamke 01 na watoto 02 wote raia wa Rwanda waliokuwa wakisafiri kutoka Tabora kuja Mbeya kwa madai ya kuwa wanaelekea Malawi kutafuta kazi kwa kutumia usafiri wa basi lenye namba za usajili T.860 BDR Kampuni ya Hamed Prince. Mbinu iliyotumika ni kupanda kwenye basi hilo kama abiria wa kawaida.
KUPATIKANA NA MALI YA WIZI.
Mnamo tarehe 24.07.2022 majira ya saa 05:30 usiku, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya msako huko Mtaa wa Mtakuja, Kata ya Utengule Usongwe, Tarafa ya Usongwe, Wilaya na Mkoa wa Mbeya ambapo katika msako huo alikamata FREDY PIUS [28] Mkazi wa Mageuzi akiwa na Pikipiki mali ya wizi yenye namba za usajili MC.471 CVX aina ya Boxer, rangi nyekundu yenye yenye Chasis namba MB2A21BX0LWG88837 na Engine namba PFXWLG06412. Mtuhumiwa amehojiwa kuhusiana na uhalali wa Pikipiki hiyo na kushindwa kutolea maelezo. Upelelezi wa shauri hili unaendelea na mara baada ya kukamilika atafikishwa mahakamani.
KUPATIKANA NA RISASI.
Mnamo tarehe 25.07.2022 majira ya saa 01:00 asubuhi, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya msako huko maeneo ya Mtakuja, Kata ya Utengule Usongwe, Tarafa ya Usongwe, Wilaya ya Mbeya na Mkoa wa Mbeya na kufanikiwa kumkamata LEODIGA MBUNDA [17] Mwanafunzi wa Kidato cha IV katika Shule ya Sekondari Mbalizi na Mkazi wa Shigamba akiwa na Risasi 01 ya Silaha aina ya AK 47 (7.62 x 39mm) ndani ya mfuko wake wa koti. Mtuhumiwa anaendelea kuhojiwa ili kubaini ni wapi alitoa na alikuwa anataka kuitumia katika shughuli gani.
Wito wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi ULRICH MATEI kwa wananchi na viongozi wa serikali za mitaa na watendaji na kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kuhakikisha wanatoa taarifa za viashiria vya uhalifu na wahalifu pamoja na kuweka mkazo wa kuimarisha vikundi vya ulinzi shirikishi @ Sungusungu vilivyopo katika maeneo yao ili kutokomeza uhalifu.
Imetolewa na,
ULRICH O. MATEI – SACP
Kamanda wa Polisi,
Mkoa wa Mbeya.
Jiandae kuhesabiwa siku ya jumanne tarehe 23 Agosti, 2022.