MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara Ndg Abdulrahman Kinana amewataka viongozi na watendaji wa Serikali kuhakikisha wanarahisisha ufanyaji wa shughuli za wananchi kwa kuwaondolea vikwazo kwa kuwa sekta binafsi inaanza na wao.
Kinana ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na wananchi wa Jimbo la Nkasi Kaskazini eneo la Lyazumbi wakati wa mapokezi ya kuanza ziara mkoani Rukwa akitokea mkoa wa Katavi.
“Serikali inafanya jitihada za kuimarisha na kuboresha mazingira ya sekta binafsi nchini ili ifanye vizuri, sasa sekta binafsi inaanza na wananchi wa kawaida. Tuwaondolee kero wananchi wetu na tuwarahisishie kufanya shughuli zao iwe ni wakulima, wafugaji, bodaboda, wamachinga au wafanyabishara.” Amesema Kinana
Akimkaribisha mkoani Rukwa Mwenyekiti wa CCM mkoa huo Ndugu Rainer Lukalah amemueleza Ndg Kinana kuwa hali ya siasa katika mkoa huo ni shwari na wanaridhishwa na kazi kubwa ya maendeleo inayofanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Kinana ameingia mkoani Rukwa ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya uimarishaji chama na ukaguzi wa utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM akiwa ameambatana na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Itikadi na Uenezi Ndg Shaka Hamdu Shaka.
Katika hatua nyingine Kinana, amewataka viongozi wa Mkoa wa Rukwa kutafuta maridhiano juu ya malalamiko ya wananchi kudai wanalazimishwa kwenda kituo kipya cha mabasi kilichojengwa nje kidogo ya Manispaa ya Sumbawanga.
Akizungumza leo Julai 26, 2022 kwenye kikao cha ndani kilichowakutanisha wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kinana amesema amepokea malalamiko kuhusu Stendi iliyopo Sumbawanga Mjini na kituo kipya cha mabasi Katumba Azimio.
“Kuna kituo cha basi kipya nimekwenda kukitembelea, nimekuta vijana wana mabango wanataka kuwe na kituo kimoja cha basi. Lakini nikiwa hapa mjini wanasema kile kituo kiwepo na cha hapa mjini kifanye kazi.
“Sasa nimekuwa na mazungumzo na Meya, nimekuwa na mazungumzo na Madiwani, nimezungumza na Mkuu wa Mkoa na wamenikubalia watakaa na kutatua manung’uniko. Haiwezekani watu wanamanung’uniko halafu tunakaa kama hatuoni.
“Kituo kile kipya kimetumia fedha nyingi, lakini stendi mpya zimejengwa katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Dar es Salaam kituo cha mabasi kimejengwa umbali wa kilomita 30, lakini hivi sasa kituo kile kimechangamka na shughuli mbalimbali zinafanyika.
“Hivyo wananchi wanachotaka kituo kijengwe lakini wakati huo huo kisiharibu maisha ya watu. Watu wanatoka safari halafu wanaambiwa wasishuke mjini, hadi Katumba Azimio na akifika huko ndio apande gari nyingine kurudi mjini.
“Sasa swali la kujiuliza hivi kuna dhambi gani dereva akisimama nikashuka? Viongozi tuko kwa ajili ya wananchi, wananchi hawako kwa ajili ya viongozi, na wananchi wako kwa ajili ya viongozi ni sehemu moja tu kwa ajili ya kupiga kura, viongozi walioko mezani wanapiga magoti wakati wa kupiga kura, lakini wakishachaguliwa wanapandisha mabega,” amesema Kinana wakati akielezea suala hilo.
Amefafanua kuwa, ujenzi wa kituo hicho kipya ni jambo zuri, la maendeleo, lakini kikubwa viongozi kukaa na wananchi na kuwaelimisha. Kuwa kiongozi sio kuwa na haki miliki ya akili, busara na kuamua, hivyo lazima tukae tushauriane, na hatuwezi kukosa njia nzuri ya kushauriana.
“Haiwezekani mara moja tu utararibu ukaondolewa na haiwezekani kwa miaka 10 kituo kipya kikabaki kama kilivyo sasa, ni vema pande zote wakanufaika, mama anayetaka kuuza kitumbua abaki apate riziki.
“Sasa niwambie tumekubaliana na viongozi watakaa na kutafuta namna nzuri ambayo haitambughudhi mtu yeyote, kila mtu aridhike na tutafute maridhiano kwa njia nzuri.
Mwisho