Na Masanja Mabula , PEMBA.
WAFUGAJI Wa Ngo’mbe wa Maziwa, Katika Shamba la Karantini ya Mifugo la Fueni Bubujiko Wilaya ya Wete Pemba, wamesema hawako tayari kuondoshwa katika eneo hilo kwa kupisha ujenzi wa kiwanja cha kufurahishia watoto, kwani wameekeza nguvu zao pamoja na kutegemea eneo hilo kwa muda usiopungua miaka 35 .
Wameyasema hayo katika kikao cha kujadili maridhiano kati yao na Mbunge wa Jimbo la Wete, kuhusiana na kupewa eneo hilo kwa ajili ya ujenzi wa kiwanja cha kufurahishia watoto.
Walisema kuwa ukiachia mbali shughuli za uzalishaji , pia eneo hilo linatumika kama ni shamba darasa kwa wafugaji wa ngombe wa wilaya nne za Kisiwani cha Pemba
“Hatuwezi kuondoka hapa kupisha ujenzi wa kiwanja cha kufurahishia watoto, kwani serikali na wafugaji watakosa kipato ikizingatiwa kiwanja kinatumika mara chache kwa mwaka lakini kwa sasa eneo hili linatumika mara kwa mara na jamii inanufaika”alisema Salum Mohammed.
Naye Asha Hamad Alawi alishauri kutafutwa eneo jengine kwa ajili ya ujenzi wa kiwanja cha kufurahishia watoto lakini eneo hilo waachie waendelee na shughuli zaao za ufugaji.
Akizungumza baada ya kusikiliza maoni ya wafugaji mbunge wa Jimbo la Wete, Omar Ali Omar, alisema ameridhia maamuzi ya wafugaj hao na kwamba yuko tayari kuunga mkono shughuli zao kwa ajili ya maendeleo.
“Uwamuzi wenu mimi Mbunge wenu nimeridhia kwani umelenga kupanua wigo wa uzalishaji sambamba na kipato chenu”alisema
Afisa tawala Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji ,Maliasili na Mkifugo, Abdalla Hamad Khamis, akizungumza kwa niaba ya Afisa Mdhamin wa Wizara hiyo amemshukuru Mbunge huyo kwa uwamuzi wake .
Shamba hilo lenye ngombe 50, na wafugaji 45 linazalisha maziwa lita 383 kwa siku na lina ukubwa wa takriban ekari 10 na linatoa huduma kwa wanajamii wa ndani na nje ya kisiwa cha Pemba..