Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani,Jumanne Sagini akizungumza na waandishi wa Habari juu ya masuala ya Usalama Barabarani katika ukumbi wa Mikutano wa ofisi ndogo ya Jeshi la Polisi,Dar es Salaam.
Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Wilbroad Mutafungwa akizungumza na waandishi wa Habari juu ya masuala ya Usalama Barabarani katika ukumbi wa Mikutano wa ofisi ndogo ya Jeshi la Polisi,Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, CPA Habibu J. Suluo akisikiliza maelekezo ya Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani,Jumanne Sagini kwenye ukumbi wa Mikutano wa ofisi ndogo ya Jeshi la Polisi,Dar es Salaam.
……………………………………
Na Mwanadishi wetu,
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Baraza la Taifa la Usalama Barabarani imetoa maelekezo yatayosaidia kudhibiti ajali za barabarani nchini. Serikali imesema kuwa hairidhishwi na takwimu za ajali barabarani zilizotokea hivi karibuni na kutoa maelekezo matano kwa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, LATRA pamoja na watumiaji vyombo vya moto na abiria kwa ujumla.
Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, Jumanne Sagini amesema kuwa Serikali ambayo inadhamana ya kulinda usalama wa raia na mali zao isingependa kuona matukio ya vifo na uharibifu wa mali za raia yakiendelea.
Naibu Waziri Sagini alielekeza LATRA na Kikosi cha Usalama Barabarani kupitia idadi ya magari madogo yaliyopewa leseni, kuendelea kufanya operesheni za kukamata magari yanayokiuka Sheria za Barabarani, kutoa elimu kwa abiria na wafanyabiashara wenye uwezo kuomba leseni za usafirishaji wa abiria kutoka LATRA kwenye maeneo ya uhitaji yakiwemo Mikoa ya Simiyu, Kagera, Kigoma, Mara na Geita.
“Serikali ambayo ina dhamana ya kulinda Usalama wa Raia na mali zao isingependa kuona matukio ya vifo na uharibifu wa mali za raia wake yakiendelea. Ni kwa msingi huo, tumemsikia mara kadhaa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akikemea na kulitaka Jeshi la Polisi kuchukua hatua madhubuti kudhibiti ajali za barabarani.
Naibu Waziri Sagini ameyasema hayo leo kwenye mkutano na waandishi wa Habari kuzungumzia masuala ya usalama barabarani uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Aidha ameipongeza Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Simiyu chini ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. David Kafulila kwa kuchukua hatua za kudhibiti matumizi ya magari yaliyosajiliwa kama teksi yanayokukiuka Sheria na kubeba abiria wengi na kwa masafa marefu.
“ Kamati hiyo ilichukua hatua hizo baada ya kujiridhisha kuwa magari hayo yamekuwa yakikiuka kwa kiwango kikubwa Sheria ya Usalama barabarani ikiwemo kubeba abiria wengi kuliko uwezo wa gari hizo, kuendesha magari kwa mwendo kasi kuliko inavyoruhusiwa” alisema.
Hatahivyo aliagiza Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani kuchukua hatua kwa askari Polisi mkoani Simiyu na nchini kwa ujumla watakaobainika wanamiliki tesksi hizo.