*************************
Balozi wa Ujerumani Nchini Tanzania Mhe. Regine Hess ameipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) Kwa juhudi kubwa inazofanya kuimarisha miundombinu ya Utalii katika Hifadhi ya Magofu ya kale ya Kilwa Kisiwani iliyopo Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi.
Pongezi hizo zimetolewa na balozi huyo Leo Julai 22, 2022 alipotembelea Hifadhi hiyo akiwa ameambatana na mumewe Bw. Collins Davison pamoja na Mkurugenzi wa Makumbusho ya Taifa Dr. Felix Chami.
Akizungumza mbele ya Kamanda wa Kituo cha Magofu ya Kale ya Kilwa Mercy Mbogellah, Mhe. Hess ameeleza kufurahishwa na kazi nzuri inayofanywa na TAWA ndani ya Hifadhi hiyo katika kuimarisha miundombinu ya Utalii hususani ujenzi wa sehemu ya kupumzikia wageni/watalii (Tourism Lounge).
Akiwa ndani ya Hifadhi hiyo, Mhe. Regine Hess alipata fursa ya Kufanya Utalii wa baharini Kwa kutumia boti la kisasa lenye kioo maalumu kinachomwezesha mtalii kuona viumbe waliopo chini ya bahari (Glass Bottom Boat) na kupata historia ya Magofu ya kale yaliyopo hifadhini humo.
Aidha Balozi Hess ameishukuru Serikali ya Wilaya ya Kilwa pamoja na TAWA Kwa mapokezi mazuri aliyoyapata Wilayani hapo mpaka kufika katika Hifadhi hiyo iliyo chini ya Usimamizi wa TAWA.
Balozi Regine Hess anaendelea na ziara yake Mkoani Lindi ambapo atatembelea vivutio mbalimbali vya Utalii vilivyopo Mkoani humo.