*********************
Jamii za Kitanzania zimetakiwa kulitumia Tamasha la Siku ya Utamaduni wa Mtanzania kama chachu ya majadiliano ya kimaendeleo na kuunga mkono jitihada za Serikali zinazolenga kuwahimiza Wananchi kujikwamua katika hali ya umaskini, ujinga na maradhi.
Hayo yamesemwa leo Julai 22,2022 na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) wakati wa ufunguzi wa Tamasha la Siku ya Utamaduni wa Mtanzania iliyowakilishwa na Jamii ya Wasafwa katika eneo la Kijiji cha Makumbusho ya Taifa jijini Dar es Salaam.
“Ni matumaini ya Serikali kuwa jamii mbalimbali zitaendelea kulitumia tamasha hili siyo tu kuonesha mila na desturi zao kwa Watanzania wenzao, bali pia kama chachu ya majadiliano ya kimaendeleo” Mhe. Masanja amesisitiza.
Amevipongeza vikundi vya Mkoa wa Rukwa na Katavi vya makabila ya Waha, Wanyasa, Jamii za Lindi na Wanamakete ambavyo kupitia tamasha hilo vimefanikiwa kuanzisha programu za kujikwamua kiuchumi hasa kilimo, ufugaji na ujasiriamali wa biashara ndogondogo.
Amefafanua kuwa kupitia tamasha hilo wananchi wanapata elimu na ufahamu juu ya desturi zilizopo na zinazofaa kudumishwa.
Pia, ameongeza kuwa kupitia tamasha hilo, Shirika la Makumbusho ya Taifa linapata fursa ya kukusanya na kuhifadhi mikusanyo ya urithi wa utamaduni unaoshikika na usioshikika ambayo ni mojawapo ya kazi zake za msingi.
Aidha, amesema Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Taasisi zake itaendelea kuhamasisha jamii kutangaza utalii wa Utamaduni ndani na nje ya nchi kwa lengo la kuurithisha kutoka kizazi kimoja hadi kingine kama dira ya Makumbusho ya Taifa inavyopambanua.
Kwa upande wake Mwenyeji wa Sherehe za Siku ya Utamaduni wa Mtanzania, Chifu Roketi Mwashinga amewataka Watanzania kuenzi mila na desturi ili kutunza maadili ya vizazi vya sasa na vijavyo.
“Vijana wa sasa hivi tusizitupe mila tutadumbukia kwenye shimo, hata kama umesoma sana ni lazima kutunza mila na desturi kwa kila kabila” amesema Chifu Mwashinga.
Tamasha la Utamaduni wa Mtanzania lilianzishwa mwaka 1994 kwa lengo la kutangaza tamaduni za jamii mbalimbali za Kitanzania na mpaka sasa takribani jamii 33 kati ya makabila 120 nchini Tanzania zimeshakutana kwa ajili ya kusherehekea tamaduni zao.