Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
SERIKALI Mkoani Pwani, imetoa Rai kwa Taasisi za Serikali zinazohusika na Uwekezaji kuwafikia Wawekezaji pamoja na kutoa Elimu wakati wakiwa kwenye hatua za awali za Uwekezaji .
“Haipendezi kukuta mwekezaji kapewa vibali karibu vyote na kukosa kimoja, Tukae na Wawekezaji tuwaeleweshe waelewe ” Amewaeleza Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge.
Mkuu huyo wa Mkoa wa Pwani,ametoa rai hiyo , wakati alipotembelea Kiwanda cha Futan Mining International Ltd ,kilichopo eneo la Visiga B Kibaha Mjini Kinachojihusisha na kuyeyusha Shaba (Copper Smelting).
Kunenge alifika kiwandani hapo kukagua na kutatua Changamoto ya Wawekezaji hao ,na kusema baadhi ya Taasisi husika za uwekezaji na watendaji zisiwe sehemu ya kukwamisha juhudi za kuinua sekta ya viwanda na uwekezaji.
“Changamoto imejitokeza wamekuja Wawekezaji wamejenga kiwanda kikubwa kimekamilika kwenye eneo la viwanda vidogo ,wamepewa Vibali vyote isipokuwa cheti cha tathimin ya Athari ya Mazingira EIA , hawawezi kuendelea na uzalishaji”.
Kunenge ameeleza kuwa Eneo hilo pia ni Eneo la Viwanda Vidogo Lakini bado kuzunguka eneo kuna wananchi wamejenga Makazi jambo ambalo ni kinyume na Mipango miji.
Amemtaka Mkurugenzi wa Mji kusimamia mipango miji “Maamuzi tuliokubaliana eneo hili lipangwe vizuri tuwaeleze wananchi Eneo hili ni Viwanda Vidogo Tutawashirikishe wananchi wasiendelee kufanya maendelezo kwenye eneo hili isipokuwa Viwanda.
Na kwa wale ambao wamepakana na Kiwanda hiki Muwekezaji yupo tayari kutoa Fidia ili aendelee na Uwekezaji” Ameeleza Kunenge.