***********************************
Na. Damian Kunambi, Njombe
Baadhi ya madereva wa magari yanayofanya kazi katika mradi wa ujenzi wa barabara inayoelekea katika mgodi wa makaa ya mawe uliopo katika kata ya Luilo wilayani Ludewa mkoani Njombe unaomilikiwa na kampuni ya Maxcoal wamedaiwa kufanya wizi wa mafuta kwenye magari hayo wanayoendesha kwa kushirikina na wananchi na kuyaingiza mtaani kwaajili ya biashara.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara mkurugenzi wa kampuni hiyo Vicent Malima mbele ya mkuu wa polisi wa wilaya ya Ludewa SSP Deogratius Massawe amesema kuwa kumekuwa na wizi wa mafuta ya Disel kutoka katika kamapuni yake na kupelekwa mtaani kwaajili ya biashara.
Ameongeza kuwa hivi karibuni walipewa taarifa na wasamalia wema juu ya wahusika wa wizi huo ambapo walifanikiwa kukama maduta zaidi ya lita 400 ambazo zilikuwa zimepakuliwa kwenye magari yao tayari kwa kufanyiwa biashara.
” Wakati tunakamata kiasi hicho cha mafuta wakati huo huo kuna mafuta mengine yalikuwa yakipelekwa manda ambayo hayo hatukufanikiwa kuyapata”. Amesema Malima.
Hata hivyo kwa upande wa wakazi wa kata hiyo wamedai kuwa wizi huo hufanywa na wageni ambao ni madereva wa mradi wa barabara unaojengwa kwa fedha za kampuni hiyo ya Maxcoal na kumkabidhi tenda mchina ambaye ndiye aliyewaleta madereva hao.
Joseph Gama ni mmoja wa wananchi hao amesema madereva hao walikuja na wenzao na kuwapangia vyumba maeneo ya jirani ambapo marafiki hao walikuwa wanayapokea mafuta na kufanya biashara.
” Mimi na baadhi ya wenzangu tuliwashuhudia wageni hao wakija na jinsi wanavyoiba mafuta hayo ndipo tukatoa taarifa kwa mkurugenzi wa kampuni ya Maxcoal hivyo tunaomba polisi mtulinde kwakuwa madereva hawa wanaweza kutugonga na gari kwa makusudi kutokana na kutoa taarifa juu yao’, Amesema Gama.
Kwa upande wake mkuu wa polisi wilaya ya Ludewa Deogratius Masawe amewataka viongozi wa kata na vijiji kuwatambua wageni wanaohamia kwenye maeneo yao sambamba na kuwataka wananchi kuendelea kuwa wazalendo na kutoa taarifa juu ya matukio ya uharifu.
” Watendaji na mwenyekiti wa kijiji wa Luilo mnapaswa kuwatambua wageni wote wanaokuja katika maeneo yenu, hii itasaidia kubaini wezi kwakuwa mtakuwa mnajua shughuli wanazofanya”, Amesema Massawe.
Pia ameaataka wananchi kuwa wazalendo kwakuwa uwepo wa miradi unasaidia kukuza uchumi wao hivyo wanapowaibia wawekezaji watapelekea kushindwa kuendwleza miaradi na uchumi wao kuzidi kudidimia.