********************
Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
Julai 15
Mwenyekiti wa Kamati ya Miradi na Ufundi ya Bodi ya Wakala wa maji safi na usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA),Mhandisi Ngwisa Mpembe ameagiza watendaji na wasimamizi kujiepusha na mlolongo mrefu wa ucheleweshaji wa fedha kwa wakandarasi wanaotekeleza miradi mbalimbali ya maji ili ikamilike kwa wakati kulingana na mikataba.
Vilevile, ametoa onyo kwa watu wanaoharibu Mazingira na miundombinu ya miradi ya mabwawa ya maji pamoja na wafugaji wanaoingiza mifugo kwenye miradi hiyo .
Akikagua mradi wa mabwawa ya maji Chole wilaya ya Kisarawe pamoja na
kitongoji cha Mjembe, Kwamduma Huko Chalinze wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani ,Mpembe na wajumbe wa kamati mbili ya ukaguzi na ufundi kutoka RUWASA ,aliiagiza fedha za wakandarasi zitoke mapema baada ya mfumo wa mwaka mpya wa fedha kufunguliwa ili miradi isikwame.
Alieleza, Rais Samia Suluhu Hassan ametenga na kutoa fedha nyingi kwenye miradi ya maji hivyo ni wajibu wa wasimamizi na watendaji kutimiza wajibu ,na kuhakikisha kwenye mikwamo mrejesho unafanyika kwa wakati.
“Mirejesho ifanyike makao makuu RUWASA haraka ili kuweza kufanya uingiliaji, kuhakikisha fedha inafika kwa wakati,Kwani unakuta muda mwingine tunatembelea miradi na kukuta wakandarasi haendelei na kazi, tatizo Nini,unaambiwa mlolongo mrefu wa ucheleweshaji fedha,”
“Nasisitiza tushirikiane katika usimamizi na utendaji,tusiwe na hadithi,hadithi nyingi,lengo letu kutimiza adhma ya Serikali kumtua mama ndoo kichwani ,watu wanywe maji safi na salama”aliongeza Mpembe.
Mpembe pia aliiagiza menejimenti ya RUWASA Mkoa kuweka chujio katika mradi wa bwawa Hilo ili kupata maji safi na salama.
Meneja RUWASA Mkoani Pwani ,Beatrice Kasimbazi alisema, wana miradi 33 yenye thamani ya Bilioni 17.9 wanayoitekeleza ambayo inajumuisha miradi nane ya fedha za Uviko 19 kati ya miradi hiyo saba imekamilika na mmoja ambao upo Mkuranga umefikia asilimia 50 hadi sasa.
Kasimbazi alibainisha, Miradi ya mabwawa inakwenda kujibu kero ya maji kwa wakazi wanaoishi maeneo ambayo Yana changamoto ya upatikanaji maji juu Wala chini hivyo Lazima kuvuna maji ya mvua.
“Maeneo haya ni sanjali na Mjembe na Chole,Kwala ambako mabwawa wanayojenga yatasaidia watu zaidi ya 10,000 ,Chole 5,890 na Mjembe watu zaidi ya 5,000 watapata maji”:
Meneja wa RUWASA Kisarawe Majid alisema , mradi wa bwawa Chole ulianza 2014 ambapo mkandarasi alifika asilimia 72 na kuvunjiwa mkataba kutokana na ucheleweshaji wa mradi mwaka 2018.
Majid alisema, kufikia 2020 RUWASA ilikabidhiwa utekelezaji wa mradi huo, kwasasa wananchi wa Chole wanufaika na mradi huo ambao umefikia asilimia 93 na ikifika September mwaka huu utakuwa umekamilika.
Katibu wa jumuiya ya mradi huo wa maji, Dickson Vedasto alieleza, chanzo kikuu cha maji ni bwawa ambalo lina uwezo wa kuzalisha mita za ujazo 3,810 kwa siku,huku wastani wa mahitaji ya maji kwa Wakazi wote katika eneo la huduma ni mita za ujazo 4,800 kwa mwezi wakati wastani wa uzalishaji wa chombo ni mita za ujazo 3,900 kwa mwezi .
Kuhusu mradi wa maji Mjembe,meneja RUWASA Bagamoyo James Kionaumela alieleza ,mradi umefikia asilimia 58 , utagharimu milioni 966 na kuanzia kwenye hatua ya kupata chanzo,pili itafuata hatua ya usambazaji wa maji na wanatarajia litakamilika mwezi ujao.
Wakazi wa kitongoji cha Mjembe, Asha Bakari na Ramadhani Hemed Walisema ,kero kubwa wanafuata maji umbali wa km 8 kwenda na kurudi na kutumia maji ya kwenye madimbwi ambayo sio salama kwao.