MENEJA Mkuu wa Chama Kikuu Cha Ushirika wa Wakulima wa Tumbaku Mkoani Tabora (WETCU) Samwel Jokeya (aliyevaa tisheti ya njano) akionesha waandishi wa habari gredi mbalimbali za tumbaku iliyoandaliwa tayari kwa ajili ya mauzo
…………………………………..
Na Lucas Raphael,Tabora
CHAMA Kikuu cha Ushirika wa Wakulima wa Tumbaku Mkoani Tabora (WETCU) kimejivunia mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 5 iliyopita kutokana na ushirikiano mzuri wa wanachama, bodi na serikali.
Akizungumza na vyombo vya habari leo Meneja Mkuu wa Chama hicho Samwel Jokeya alitaja mafanikio hayo kuwa ni kuongeza idadi ya wanachama ambao ni vyama vya msingi, kutoka vyama 56 vya awali hadi kufikia 101.
Alisema vyama hivyo awali vilikuwa havilimi zao hilo, lakini baada ya kujiunga sasa vinalima kwa wingi na vinapata mikopo ya mabenki kama wakulima wengine na kunufaika na masoko yaliyopo sasa.
Alitaja mafanikio mengine kuwa ni kuongezeka kwa mapato ya Chama kutokana na uwekezaji wa hisa wa kiasi cha sh mil 24 katika benki ya CRDB ambapo kila mwaka hujipatia gawio la kati ya sh mil 500 hadi 800.
Aidha kuhusiana na ushuru wa zao hilo alisema wanapata kati ya sh mil 400 hadi 800 kila mwaka mapato ambayo yamekuwa kichocheo kikubwa cha kuboreshwa shughuli za wakulima na huduma nyinginezo.
Jokeya alibainisha kuwa uwepo wa idadi hiyo ya vyama vya msingi umesaidia Chama kulipa kodi kubwa ya serikali kuliko taasisi nyingine yoyote hivyo kuchochea kasi ya maendeleo wananchi.
Aliongeza kuwa Chama hicho kinachosimamia wakulima wa Mikoa 4 ya kitumbaku katika Mkoa huo, yaani Sikonge, Tabora Manispaa, Uyui na sehemu ya Nzega pia kimefanikiwa kutengeneza fursa za ajira kwa vijana katika maeneo yao.
‘Wakati tukiendelea kutafuta njia rahisi ya kupata pembejeo naomba kila mkulima afanye maandalizi mapema ya kwa ajili ya msimu mpya wa kilimo ikiwemo kujenga mabani ya kutosha na stoo ya kuhifadhia tumbaku yao’, alisema.
Mwenyekiti wa Bodi ya WETCU Hamza Kitunga alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri mwenye dhamana ya Kilimo Hussein Bashe kwa jinsi wanavyojali na kutetea wakulima ikiwemo kuwatafutia masoko ya uhakika ndani na nje ya nchi.
Alifafanua kuwa katika msimu uliopita walikisia kuzalisha kiasi cha kilo mil 16 za zao hilo lakini wakapata kilo mil 14 na matarajio yako katika msimu huu ni kuzalisha kati ya kilo mil 24 hadi 30 na zote ana uhakika zitanunuliwa.
Alisisitiza kila mkulima kufuata kanuni za kilimo bora ili kuongeza uzalishaji hasa ikizingatiwa kuwa serikali imeshawahakikishia soko lipo na tumbaku yote itakayozalishwa mwaka huu itanunuliwa.